Wabunge wote wa vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa, wamejitoa kwenye kamati ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi baada ya Ikulu kuwanyima kibali Mwita Waitara(Chadema) na Savelina Mwijage (CUF) kwenda Marekani na badala yake kumruhusu Mbunge wa CCM, John Kanyasu waliyepaswa kwenda naye.

Waitara ambaye ni Mbunge wa Ukonga amewaambia waandishi wa habari kuwa waliteuliwa kwa barua na Spika wa Bunge, Job Ndugai kushiriki mkutano wa Ngazi ya Juu ya Maamuzi kuhusu masuala ya Ukimwi duniani uliopangwa kufanyika jijini New York Marekani kwa siku mbili lakini hivi karibuni amepigiwa simu na kuambiwa kuwa Ikulu imetoa kibali kwa mbunge mmoja tu, John Kanyasu.

“Nikiwa Tarime nilipata simu kutoka kwa Patson kwamba, Naibu Spika alipokea simu kutoka Ikulu kuwa imezuia vibali vyetu vya kwenda Marekani na badala yake Kanyasu ameteuliwa,” alisema Waitara.

“Tunashangaa, kuteuliwa tuliambiwa kwa barua, lakini kukataliwa tuliambiwa kwa simu,” aliongeza.

Alisema kuwa uamuzi huo umefanyika kwakuwa Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson hawapendi wabunge wa Upinzani kutokana na mgogoro uliopo hivi sasa kati yao.

Naye Mbunge wa jimbo la Vunjo, James Mbatia aliushangaa uamuzi huo na kueleza kuwa Waziri Mkuu aliwaeleza wabunge kuwa Wabunge hawapaswi kuomba kibali Ikulu cha kusafiri kwenda nje ya nchi.

“Mimi mwenyewe nimeshawahi kusafiri zaidi ya mara tatu mbona sijawahi kuomba kibali kutoka Ikulu?” Mbatia anakaririwa.

Akijibu malalamiko hayo, Katibu wa Bunge, Thomas Kashililah alihoji haraka waliyonayo wabunge hao wakati tayari wameshawasilisha malalamiko yao dhidi ya Naibu Spika na wanasubiri majibu.

Mwanamuziki wa Marekani auawa kwa risasi kwenye tamasha lake
mavazi yawakutanisha Mlimani City mall na wateja wake siku tatu.