Wabunge wa Chama Cha Mapinzudi (CCM) leo wamempongeza Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Professa Mussa Assad kwa kueleza kuwa ana nia ya kuitikia wito wa Spika wa Bunge, Job Ndugai.

Mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda, amezungumza kwa niaba ya wabunge wa chama hicho na kueleza kuwa hatua ya CAG ni ya kiungwana.

“Sisi kama wabunge wa CCM tuna imani kuwa hatua hii itaendelea kudumisha na kuboresha mahusiano kati ya Ofisi ya CAG na Ofisi ya Bunge kwa maslahi ya Umma,” amesema Mapunda.

Aidha, wamempongeza Spika Ndugai kwa hatua aliyoichukua dhidi ya kauli ya awali ya CAG, wakieleza kuwa alichokifanya ni kulinda heshima ya mhimili huo.

Sakata la CAG kuitwa na Spika wa Bunge mbele ya Kamati ya Bunge limekuwa gumzo mitandaoni, ambapo hivi karibuni Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe akisaidiana na mwanasheria wake, Fatma Karume waliwasilisha shauri Mahakama Kuu kwa nia ya kufungua kesi ya kikatiba kupata tafsiri ya Ibara ya 143 (6) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu mamlaka ya CAG.

Aidha, CAG alitoa msimamo wake akieleza kuwa ana nia ya kuitikia wito wa Spika Ndugai kufika kwenye Kamati ya Bunge Januari 21.

Hata hivyo, CAG alitetea hoja yake ya kuliita Bunge kuwa ni dhaifu akisema kuwa hiyo ni lugha ya kawaida kwa wakaguzi na kwamba haikuwa na nia ya kulidhalilisha Bunge.

Alitoa kauli hiyo alipokuwa anahojiwa na chombo cha habari cha Umoja wa Mataifa akiwa nchini Marekani ambapo alisema kama Bunge halifanyii kazi ripoti anazoziwasilisha kwao huo ni kwake ni ‘udhaifu wa Bunge’.

Wafanyabiashara Dodoma hatarini kupata Magonjwa
Watuhumiwa 6 ugaidi Nairobi wapandishwa kizimbani