Vutankuvute ya hoja ya Bunge kurushwa au kutorushwa ‘Live’ na vituo vya runinga pamoja na radio nchini imepigiwa kura za sauti Bungeni ambapo wabunge wa CCM walitaka Bunge lisirushwe moja kwa moja kwa vikao vyote wakiwafunika kwa wingi na sauti wale wa Ukawa waliotaka Bunge kurushwa moja kwa moja.

Uchaguzi huo unaofanywa pale Mwenyekiti anapoamua kuwahoji wabunge kuhusu uungaji mkono au kutounga mkono hoja iliyowasilishwa, ulifanyika hivi karibuni Bungeni mjini Dodoma pale Bunge hilo lilipokaa kama Kamati.

Wabunge wa CCM walivutana na wenzao wa Ukawa, wakieleza kuwa hakuna haja ya kurusha Bunge moja kwa moja wakieleza kukurushwa au kutorushwa Live kwa Bunge hakumuongezei kitu chochote Mbunge jimboni kwake.

 

Hali hiyo ilifikiwa baada ya Mbunge wa Malindi, Ally Salehe (CUF) kutoa hoja akitaka Bunge kushikilia mshahara wa Waziri Mkuu kwa madai kuwa kuzuia Bunge kurushwa ‘live’ ni kinyume na utawala bora na haki ya kupata habari.

Hoja hiyo iliungwa mkono na wabunge wa Ukawa na kuchangiwa kwa kuungwa mkono na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Msigwa, Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko na Mbunge wa Tanga Mjini, Mussa Mbarouk.

Hata hivyo, upande wa CCM unaopinga hoja hiyo uliongezwa nguvu na Peter Serukamba (Kigoma Kaskazini), Kangi Lugola (Mwibara), Hawa Ghasia (Mtwara Vijijini) pamoja na Waziri Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki.

Kutokana na hatua hiyo, Wabunge wa vyama vya upinzani wameanzisha njia mbadala kwa kujirekodi kwa kutumia simu zao pale wanapochangia na kuzisambaza sauti hizo kwenye mitandao ya kijamii na redio zilizo katika majimbo yao.

Wakuu wa Mikoa, RAS marufuku Bungeni
Rais Magufuli ashusha neema kwa wafanyakazi