Wabunge wa vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa, wametolewa nje ya Bunge baada ya kupiga kelele wakati rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli alipoingia bungeni akiambatana na rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.

Wabunge hao awali walitoa msimamo wao wa kutokubali Dk Ali Shein kuhudhuria Bunge hilo wakati rais atakapoingia Bungeni kulihutubia Bunge kwa kuwa hawamtambui kama rais wa Zanzibar kwani kwa mujibu wa Katiba muda wake umekwisha.

Kelele za zomeazomea ziliibuka ghafla wakati Rais alipoingia na Dk Shein hali iliyoondoa utulivu wa Bunge hivyo walinzi waliingilia kati na kuwataka kutoka nje ya Bunge hilo.

Hata hivyo, Mbunge pekee wa upinzani, Zitto Kabwe (ACT – Wazalendo) alibaki ndani ya Bunge kwa utulivu na kuendelea kusikiliza hotuba ya Rais.

Awali, wabunge hao walimuandikia barua Spika wa Bunge wakihoji uhalali wa hotuba ya Rais bungeni endapo Dk Shein atahudhuria Bunge hilo kama Rais wa Zanzibar.

Ukawa wameendelea kushinikiza Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Zanzibar (NEC) kumtangaza mshindi wa nafasi ya Urais wa Zanzibar, huku mgombea wa CUF Maalim Seif Sharif Hamadi akidai kuwa ameshinda kutokana na kura halali alizokusanya kwenye vituo vyote.

 

 

Fid Q: Nimependelewa Mno Na Coke Studio
Kilimanjaro Stars Yawasili Salama Addis Ababa