Kambi rasmi ya upinzani imepanga kufanya vikao vya kujadili suluhu ya kudumu ya mgogoro na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson uliosababisha wabunge wanaounda Ukawa kususia vikao vinavyoendeshwa na kiongozi huyo.

Vikao hivyo vinapangwa kufanyika wakati mkutano wa nne unaotarajiwa kuanza rasmi kesho, baada ya kuahirishwa mwishoni mwa Juni mwaka huu wakati wa mkutano wa Bajeti. 

Mbunge wa Vunjo (NCCR- Mageuzi), James Mbatia alieleza jana kuwa uamuzi wa kufanya vikao hivyo umefikiwa baada ya upinzani kukaa kikao na viongozi wa dini Agosti 24 mwaka huu ili kutafuta suluhu ya kudumu.
“Kikao cha kwanza tutakaa kamati ya uongozi ya wabunge wa upinzani kujadili suala hilo na baadaye tutamaliza na kikao cha wabunge wote ili kubaini njia endelevu za kumaliza jambo hilo,” alisema Mbatia ambaye ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi.
Wabunge wa Ukawa wamekuwa wakisusia vikao vinavyoendeshwa na Naibu Spika kwa madai ya kutoridhishwa na uongozi wake tangu Mei mwaka huu, baada ya Dk Tulia kukataa kujadili hoja ya kufukuzwa wanafunzi zaidi ya 8,000 stashahada ya ualimu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).
Hata wakati wakisubiri kufanyika vikao hivyo ambavyo Mbatia hakutaka kuelezea kwa undani, upinzani ulitangaza kurudi bungeni baada ya mkutano wao na viongozi wa dini.
Katika mkutano na wanahabari Agosti 25, Mbatia kwa niaba ya vyama vilivyoshiriki mkutano huo wakiwamo ACT-Wazalendo, alisema wangejadiliana namna ya kufanikisha jambo hilo kama sehemu ya kutii ushauri wa viongozi hao wa kiroho.
Hata hivyo, haijawekwa bayana iwapo kesho Ukawa wataendelea na vikao hata kama Dk Tulia ataendelea kuongoza kiti hicho ama la.

Mbatia alisema jana kuwa watatoa taarifa rasmi leo namna vikao hivyo vitakavyofanyika na siku husika.

Kuhusu kupata taarifa ya mwenendo wa mchakato wa kutafuta maridhiano ulioelezwa na Spika Job Ndugai hivi karibuni, Mbatia alisema hawajapata chochote na wao wanasikia kwenye vyombo vya habari kama wengine.
Alipoulizwa ni lini vikao vya maridhiano kati ya pande hizo ya taanza, Ofisa Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bunge, Owen Mwandumbya alisema Spika anatarajiwa kufika ofisini leo na kwamba kama ataona kuna haja ya kufanya hivyo atapanga utaratibu wa namna anavyoona inafaa.

Biashara na Uwekezaji Wasisitizwa Katika Mkutano wa G20
Serikali Kuwapeleka Watoto Yatima Jeshi la Kujenga Taifa JKT