Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jana walikubali kukatwa posho ya siku nzima ili fedha hizo zitumike kuwasadia waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea wiki iliyopita katika mikoa ya Kanda ya ziwa.

Tetemeko hilo lililikuwa na ukubwa wa 5.7 kwa kipimo cha ritcher lilisababisha vifo vya watu 17 na majeruhi zaidi ya 250 na kuharibu nyumba zaidi ya 1,250.

Wakitoa mchango wao baada ya kutokea mvutano wa hoja baina ya wabunge hao na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson kuhusu kuahirisha Bunge na kujadili suala la maafa hayo, wabunge hao walioeleza kutoridhishwa na hatua zinazochukuliwa na Serikali kusaidia waathirika hao hadi jana, waliridhia wazo lililotolewa na Mbunge wa Mlalo (CCM), Rashid Shangazi kutoa shilingi 220,000 kila mmoja ambayo ni posho ya jana kuwchangia waathirika wa tetemeko hilo.

Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema) ambaye ndiye mbunge pekee wa upinzani aliyepata nafasi ya kuchangia hoja hiyo, alisema kuwa ingawa chama chake tayari kilikuwa kimeweka utaratibu wa kila mbunge kuchangia shilingi 100,000, wanaridhia pia kukatwa posho ya kikao cha jana kuwashika mkono wahanga wa janga hilo.

Akitoa taarifa Bungeni kuhusu tetemeko hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene alisema kuwa wameagiza Wakurugenzi wa Manispaa ya Bukoba kuzifunga shule za Ihungo na Nyakato zilizoharibiwa na tetemeko la ardhi kwa kuwa zina hali mbaya.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jana alichangisha zaidi ya shilingi bilioni 1.4 kutoka kwa wafanyabiashara na mashirika mbalimbali kusaidia waathirika wa tetemeko hilo.

Ripoti Yatolewa Ufaransa na Uingereza Zilichangia kumng'oa Gaddafi Libya
Marekani Kupeleka Misaada Ya Kijeshi Israel