Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wamepinga kipengele cha muswada wa marekebisho ya Sheria ya Utumishi wa Umma kilichotaka Serikali kupitisha posho na mishahara yao na ya watumishi wa mahakama.

Azimio hilo la wabunge lilikuja baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju kueleza kuwa Muswada wa Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2016 unapendekeza kuongeza kifungu kipya cha 9A kinachoweka sharti kuwa Taasisi, Wakala au Tume za Serikali hazitakuwa na mamlaka ya kuidhinisha mishahara na posho kwa watumishi wa taasisi hizo, badala yake kibali cha yote hayo kitatolewa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais (Utumishi).

“Tume ya utumishi wa Bunge na Tume ya Utumishi wa Mahakama zipewe uhuru kusimamia upangaji wa mishahara, posho na marupurupu,” alisema Mohammed Mchengerwa wakati akiwasilisha maoni ya Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria.

Baada ya kuwasilisha mapendekezo hayo, Mwanasheria Mkuu alieleza kuwa Serikali imeridhia na kwamba ibara hiyo imefutwa na kuandikwa upya.

Alisema baada ya marekebisho, masharti hayo ya kuomba kibali kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais (Utumishi) hayatumika kwa Bunge, Mahakama, Majeshi yote nchini pamoja na Idara ya Usalama wa Taifa.

Masaju alisema kuwa marekebisho hayo yamelenga katika kuwianisha mishahara, posho na marupurupu mengine kwa watumishi wa umma.

Live: Matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Rais Marekani
Ali Kiba ataka MTV EMA kueleza kwanini hawakumpa tuzo iliyoenda kwa Wizkid