Huenda Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania likawa bunge lenye ushindani mkubwa wa kila mbunge kutaka kuchangia mijadala, baada ya Uongozi wa Bunge kufikiria kuwalipa wabunge hao kutokana na wanachochangia bungeni badala ya kutumia mahudhurio.

Pendekezo hilo lilitolewa hivi karibuni na kiti cha Spika, kilichoeleza kuwa ipo haja ya kubadili kanuni za bunge ili posho zilipwe kutokana na namna wabunge wanavyoshiriki katika shughuli za Bunge badala ya kutumia daftari hilo.

Mapendekezo hayo yalikuja baada ya Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) kuomba muongozo kufuatia hatua ya Wabunge wa Upinzani kuingia Bungeni na kukaa kimya bila kuchangia mijadala inayoendelea wakati wanaendelea kulipwa posho na mishahara kwa kigezo cha mahudhurio yao.

Wabunge wa kambi ya upinzani wanaendesha mgomo baridi kupinga hatua za Bunge kukataa kurushwa moja kwa moja kupitia Televisheni ya Taifa na vituo binafsi, vikao vyote vya Bunge vinavyoendelea mjini Dodoma. Pia wanapinga hatua wanazodai Serikali imeingilia kazi za Bunge na uvunjifu wa sharia ikiwa ni pamoja na Serikali ya Awamu ya Tano kufanya kazi bila muongozo rasmi kwa mujibu wa Katiba.

Hata hivyo, Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson alieleza kuwa malipo kwa Wabunge hufanywa kutokana na mahudhurio ya wabunge na sio kwa kuchangia kwani inaterajiwa kuwa Mbunge anapohudhuria atawajibika majukumu yake ipasavyo.

““Kimsingi kuhudhuria bungeni pekee siyo njia inayopendeza kwa kuwa mbunge anapofika bungeni anatarajiwa atekeleze majukumu yake yalivyoainishwa katika Ibara ya 63. Tabia hii ya kutochangia mijadala na kuzunguka zunguka bungeni haikubaliki na haitakiwi kuendelea, kila mbunge atekeleze wajibu wake na sio anahudhuria ili alipwe posho,” alisema Dk. Tulia.

Magaidi wapanga kumteka Manny Pacquiao, Rais Wa Ufilipino anena
Prince abainika kuwa na Ukimwi siku chache kabla ya kifo chache