SERIKALI imeridhia wachezaji wa kigeni wanaocheza soka la kulipwa nchini kubakia 10 kwa kila klabu inayotaka kusajili kama ilivyokuwa awali.

Akitangaza uamuzi huo jana, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrisons Mwakyembe, amesema serikali imekubali kuendelea kuruhusu idadi 10 ya wachezaji wa kigeni baada ya kuzingatia maoni yaliyotolewa na wadau wengi.

Dk. Mwakyembe alisema kati ya watu 977 waliotoa maoni kwa njia mbalimbali, 809 wametaka idadi ya wachezaji 10 iendelee kuwapo.

Ikumbukwe kuwa wizara hiyo ilianzisha mchakato wa wadau kutoa maoni yao ya kutaka kuendelea kuwa na wachezaji 10 wa kigeni au ipunguzwe.

Hata hivyo, waziri huyo amesema kuwa idadi ya wachezaji wanaotakiwa kuanza mechi itabaki chini ya Baraza la Michezo Nchini (BMT). Pia amesema bado wizara kwa kushirikiana na BMT na wadau wa soka watakaa kujadili aina ya viwango vya wachezaji wanaopashwa kusajiliwa na kucheza nchini.

“Angalau nchi zilizopo katika nafasi 50 kwa Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) ndiyo tusajili huko hata Daraja la Kwanza, ingawa bado si sheria ni maoni tu. Ni vema pia aina ya wachezaji watakaosajiliwa wawe na uwezo mkubwa,” alisema.

Aidha, wizara imeagiza kuwa watu wanaoajiriwa nchini wawe na ulazima wa kujifunza, au kufundishwa lugha ya Kiswahili.

Papaa Zahera kocha mkuu Gwambina FC
Amchinja mtoto, kisa wivu wa mapenzi