Baadhi ya wachezaji wa timu ya taifa ya Argentina, wameutaka uongozi wa shirikisho la soka la nchi hiyo kumuondoa kocha Jorge Sampaoli na kumteua mkuu mwingine wa benchi la ufundi, kuelekea mchezo wao wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya Nigeria.

Kwa mujibu wa chombo cya habari cha Argentina Sebas Tempone, ombi hilo la baadhi ya wachezaji kwa viongozi wa shirikisho, limekuja kufuatia kufungwa katika mchezo wa usiku wa kuamkia leo dhidi ya Croatia.

Pasina kutaja majina ya wachezaji waliowasilisha ombi hilo, chombo hicho cha habari kimeleza kuwa, kocha Sampaoli analalamikiwa kutokana na falsafa yake ya ufundishaji, ambayo imekua haiwajengi wachezaji katika mfumo wa mapambano na kuleta umoja baina yao.

Chombo hicho ha habari kimeeleza kuwa, sababu nyingine zilizotolewa katika ombi la wachezjai hao, ni kutaka kuwa na mtu mwingine katika benchi lao la ufundi ambaye wanaamini anaweza kuwasaidia katika harakati za kupambana kwenye mtanange dhidi ya Nigeria utakaochezwa juma lijalo.

Hata hivyo haijafahamika wachezaji hao wamempendekeza nani awe mkuu wa benchi la ufundi, endapo ombi lao litakubaliwa na viongozi wa shirikisho la soka nchini Argentina.

Jorge Sampaoli mpaka sasa ameshindwa kukiwezesha kikosi cha Argentina kupata ushindi katika michezo ya kundi D, baada la kulazimishwa sare ya bao moja kwa moja dhidi ya Iceland juma lililopita, na jana ameambulia kichapo cha mabao matatu kwa sifuri.

Mustakabali wa kikosi cha Argentina utafahamika mara baada ya mchezo wa leo wa kundi D kati ya Nigeria na Iceland unaotarajiwa kuchezwa saa kumi na mbili jioni kwa saa za Afrika Mashariki.

Endapo Nigeria watashinda mchezo huo, Argentina watakua na matumaini ya kufuzu kama atafanikiwa kushinda mchezo wao wa mwisho dhidi ya wawakilishi wa Afrika (Nigeria), na kama Iceland watashinda matumaini kwa mabingwa hao wa mwaka 1986 yatafifia. Na kama wawili hao watapata matokeo ya sare yoyote pia Argentina watakuwa na matumaini ya kufuzu.

Barcelona, Gremio kukamilisha dili la Arthur de Oliveira Melo
Habari kubwa katika magazeti ya leo Juni 22, 2018