Shirikisho la Soka Zanzibar ‘ZFF’ limewaonya Wachezaji wa Klabu za Ligi Kuu visiwani humo ‘PBZ Premier League’ pamoja na Ligi Daraja la kwanza Kanda ya Unguja na Pemba, kutojihusisha na kucheza Michuano ya Mitaani (NDONDO Cup) kwa kipindi chote cha Mapumziko ya Mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Taarifa iliyotolewa na Idara ya habari na Mawasiliano ya ZFF leo Ijumaa (March 24, 2023) imeeleza kuwa, Mchezaji yeyote atakaebainika kucheza Michuano isiyo rasmi (Ndondo Cup) kwa kipindi cha Ramadhan, Hatua kali zitachukuliwa dhidi yake kwa mujibu wa kanuni ya Mashindano 2022-23.

“ZFF inawaomba Waanzilishi wa Ndondo Cup katika kipindi hichi cha Ramadhan kufuata Miongozo yote ya kanuni ya Mashindano na kutowahusisha Wachezaji wa Ligi kuu na Daraja la kwanza kwenye michuano yao hiyo.”

“Mwisho kabisa, ZFF inawataka Wachezaji kufuata Miongozo ya Mazoezi ya Timu zao, ili kujiepusha na Athari yeyote ambayo inaweza kujitokeza kabla na Baada ya kurejea kwa Ligi na Mashindano mbali mbali ya ZFF, baada ya kupita Wiki 4 za Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.” Imeeleza taarifa hiyo

Shirikisho la Soka visiwani Zanzibar ‘ZFF’ limetangaza kusimamisha Ligi zote ili kupisha ibada ya mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhana, ambayo rasmi ilianza jana Alhamis (Machi 23, 2023).

Nape awakubali waleta mageuzi sekta ya Mawasiliano
Benchi la ufundi, Wachezaji Azam FC wajitafakari