Serikali kupitia Tume ya Madini imetoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo wa madini 350 katika mikoa ya Arusha na Katavi yaliyolenga kuwajengea uwezo wa kutumia njia bora na za kisasa ili kuwawezesha kuachana na matumizi ya Zebaki yanayoathiri mazingira.

Hayo yamesemewa na Mkaguzi wa Madini na Mazingira wa Tume hiyo, John Mataro katika Maonyesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa jijini Dar es Salaam (DITF) yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere, ambapo amesema kuwa Tume hiyo imekusudia kuhakikisha kuwa suala la uhifadhi na utunzaji wa mazingira linapewa kipaumbele na kila mchimbaji wa madini nchini.

Amesema kuwa Ofisi hiyo imekuwa ikitoa miongozo mbalimbali kupitia sheria zilizopo kwa ajili ya kuwaelimisha wachimbaji wadogo, na kampeni hiyo itakuwa endelevu ili kuhakikisha kuwa maeneo yote yanayotumiwa na wachimbaji madini hususani wachimbaji wadogo yanazingatia maelezo hayo ili kuweza kuwa na uchimbaji endelevu na salama.

“Malengo ya Serikali ni kuhakikisha kuwa wachimbaji wetu wanaweza kupata kipato cha kutosha ili kuweza kujikwamua kiuchumi, na hili litafanyika kwa kuhakikisha kuwa tunajenga mazingira yenye usalama wa hali ya juu katika maeneo yote ya uchimbaji yaliyopo nchini,” amesema Mataro.

Aidha, Mataro ameongeza kuwa Tume hiyo kwa kutambua mchango wa wachimbaji wadogo nchini imekuwa ikiwajengea uwezo wachimbaji hao kwa kujenga mazingira wezeshi ikiwemo kupata mikopo nafuu kupitia taasisi za kifedha ikiwemo Benki, hatua inayolenga kuwapa morali na uwezo wa kumiliki vifaa bora na vya kisasa kwa ajili ya uchimbaji wa madini.

Hata hivyo, amesema kuwa mara kwa mara Tume hiyo imekuwa ikifanya ziara katika migodi mbalimbali iliyopo nchini yenye lengo la kuwakumbusha wachimbaji wote hususani wachimbaji wadogo kuzingatia miongozo mbalimbali ikiwemo kuwepo matangazo mbalimbali ya tahadhari katika maeneo ya uchimbaji ili kuweza kutoa taarifa kwa wahusika wanaofika katika maeneo hayo kwa mara ya kwanza.

TTCL yaimarisha huduma zake, yavuna wateja lukuki
Jeshi la Sudan ‘lakubali yaishe’, wananchi washerehekea