Wachimbaji wawili wa Dhahabu katika kijiji cha Izumbi, Sangamba Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya, wamefariki dunia baada ya kufukiwa na kifusi cha udongo katika Mgodi wa Mwembe.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei amesema kuwa tukio hilo limetokea siku ya Julai 2, 2019 majira ya saa 10 jioni, ambapo wachimbaji hao walifariki baada ya kuangukiwa na kifusi kilichochanganyika na mawe hali iliyopelekea kukosa hewa.

”Wakati wanafanya shughuli hizo, waliangukiwa na kifusi cha udongo mchanganyiko na mawe na kusababishia kifo baada ya kukosa hewa. Mwamba huo unamilikiwa na mtu mmoja anayejulikana kwa jina la Mwembe Msemakweli, na sisi kama jeshi la polisi baada ya kupata taarifa hizo, tulifika eneo la tukio na kuthibitisha na marehemu walifariki wakati wanakimbizwa Zahanati,” amesema Kamanda Matei.

Aidha Kamanda Matei ametoa rai kwa wale wanaofanya shughuli za uchimbaji, akiwataka kuwa makini wakati wa kufanya shughuli zao, na kwamba shughuli ya kupanga mbao za kuzuia vifusi waifanye kabla hawajaingia ndani ya shimo badala ya kupanga wakiwa ndani ya shimo.

Hata hivyo, kamanda Matei amewataja waliofariki kuwa, ni Zakayo Muyunga na Ayoub Mpimbi wote wakazi wa Izumbi.

Wema mambo bado magumu, aachiwa, akamatwa tena
Nigeria kusaini makubaliano ya Afrika kuwa eneo huru la biashara