Aliyekua kocha mkuu wa timu ya taifa ya Uingereza Sam Allardyce, huenda akarejea Stadium Of Light kwa ajili ya kukinoa kikosi cha klabu ya Sunderland ambacho kwa sasa kipo chini ya utawala wa meneja David Moyes.

Tetesi za kurejea kwa Big Sam ambaye alitangaza kujiuzulu nafasi ya kocha mkuu wa Uingereza majuma matatu yaliyopita, zimeibuliwa na gazeti la The Sun kwa kuihusisha kampuni ya biashara ya kichina (Chinese consortium) ambayo imeonyesha nia ya dhati ya kuinunua klabu hiyo.

Mmiliki wa sasa wa klabu ya Sunderland Ellis Short, bado ana matumaini makubwa na Moyes lakini changamoto ya uwepo wa kufanyika kwa biashara ya kuiuza The Black Cats huenda ikaharibu imani ya meneja huyo kutoka nchini Scotland.

Taarifa hizo zimeeleza kuwa wamiliki wa kampuni ya Chinese consortium wamefanya uchunguzi wa kina na kubaini uwezo wa Big Sam, na wanajipanga kumpendekeza katika sehemu ya mazungumzo yao ya kibiashara ya kutaka kuinunu klabu ya Sunderland.

Allardyce, aliondoka klabuni hapo miezi minne iliyopita, baada ya kuhakikishiwa ajira na chama cha soka nchini Uingereza FA, kufuatia kujiuzulu kwa aliyekua kocha wa The Three Lions Roy Hodgson baada ya kushindwa kukiongoza vyema kikosi chake wakati wa fainali za Euro 2016 zilizofanyika nchini Ufaransa.

Lakini mwanzoni mwa mwezi huu Big Sam alilazimika kujiuzulu nafasi ya kocha mkuu wa kikosi cha timu ya taifa ya Uingereza, kufuatia sakata la uvujishaji siri za FA, lililoibuliwa na gazeti la Daily Telegraph.

AS Roma Wapanga Kubomoa Ukuta Wa Man City
Dk Slaa aibukia Sakata la Gambo na Lema, amkingia kifua Lema