Serikali imewataka wadau wa michezo hapa nchini  kujitokeza na kuwa mstari wa mbele kushiriki na kudhamini michezo mbalimbali nchini.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Anastazia Wambura alipokuwa akizungumza na  wanamichezo wanaokwenda kushiriki mashindano ya Olimpiki kwa mwaka 2016 yanayofanyika Jijini Rio dejaneiro nchini Brazil.

Hata hivyo Mhe. Anastazia Wambura amesema kuwa wadau wa michezo wamekuwa wakishirikiana na Serikali sio katika suala la michezo pekee hata katika habari na Sanaa na amewapongeza kampuni ya ving’amuzi ya Multichoice Tanzania (DSTV) na Bodi ya Utalii katika azma yao ya kuunga mkono maendeleo ya sera ya michezo nchini.

“Napenda kuwashukuru wadau wetu Dstv na Bodi ya Utalii, nawapongeza kwa kuona fursa hii muhimu na kuitumia kuwatia moyo wawakilishi wa nchi yetu katika michezo ya Olimpiki kwa mwaka 2016 mueendelee kuiunga mkono Serikali katika kutekeleza sera ya maendeleo ya Michezo ili kufikia malengo” alisema Mhe. Anastazia.

Aidha amewataka wawakilishi wa Olimpiki kutumia fursa hii ya wadau wa michezo waliojitokeza kuwaunga mkono ikiwemo Bodi ya Utalii kutangaza utalii wa Tanzania kwa mataifa  mengine watakayo kutana nayo katika mashindano ya Olimpiki nchini Brazil.

Kwa upande wake Mkurungezi Mkuu wa Multichoice Tanzania Bw.Maharage Chande ameishukuru Serikali kwa kuwapa fursa ya kushirikiana na timu ya Olimpiki kuitangaza michezo na kuitangaza Tanzania kimataifa na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuendeleza michezo nchini

Wakulima, Wafugaji na Wavuvi wataongeza Ari ya Uzalishaji Viwandani - Majaliwa
Video: Pestana CR7 Hotel ya Cristiano Ronaldo