Shirikisho la soka nchini (TFF) pamoja na viongozi wa klabu za Ligi Kuu Bara wamekutana kujadili mambo mbalimbali ya maendeleo ya soka nchini ikiwemo kupitia kanuni za ligi na Kombe la FA.

Mbali na hayo pia wanajadili juu ya mkataba wa Azam Tv ambao umemalizika ili kuona ni jinsi gani wataweza kumshawishi mdhamini huyo awekeze zaidi kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.

Kikao hicho ambacho kimeanza jana katika ofisi za shirikisho hilo zilizopo Uwanja wa Karume hakikumalizika jana Ijumaa na kimeendelea leo Jumamosi.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho zilieleza kuwa baadhi ya viongozi wa klabu walipendekeza pia kuwa katika marekebesho ya kanuni hizo klabu ziliruhusiwe kusajili wachezaji kumi wa kigeni badala ya saba, ingawa maombi hayo yalidaiwa kupingwa.

“Kuna mambo mbalimbali yanajadiliwa ila kubwa ni marekebisho ya kanuni za Ligi Kuu pamoja na Kombe la FA. TFF wameona tujadili kwa haraka maana mkataba wa Azam umemalizika na wataka kukaa mezani kujadili upya hivyo huwezi kujadili kwa kanuni za zamani.

“Pia kuna wadau walikuja na maombi tofauti ya kuongezewa wachezaji na kupendekeza wachezaji wa kigeni watakaosajiliwa ni wale wanaotoka kwenye timu zao za Taifa na wawe kumi ila hili halijapitishwa,” kilisema chanzo hicho

Azam waliingia mkataba wa miaka mitatu ambao umemalizika mwaka huu ambapo kila timu ilikuwa ikipewa Sh 100 milioni kwa msimu.

Mafarao Wazima Ndoto Za Taifa Stars Fainali Za Afrika 2017
Uchaguzi Wa Young Africans: Manji Na Wenzake Wavuka Hatua Ya Kwanza