Jitihada ambazo zimekuwa zikifanywa na Asasi za kiraia (AZAKI), katika kuimarisha ushirikiano miongoni mwa wadau mbalimbali wa sekta hiyo zinatambuliwa na sekta binafsi kama sehemu muhimu ya kuharakisha maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Kauli hiyo imetolewa Agosti 18,2022 Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela katika uzinduzi wa Wiki ya Asasi za Kiraia (AZAKI) 2022 ambapo alikuwa mgeni rasmi.

Amesema, ushirikiano baina ya Aasi za kiraia na Sekta Binafsi unaweza kutoa suluhisho la changamoto za maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa ufanisi, kuliko kila Taasisi kufanya kazi kivyake.

“Kwa bahati mbaya kumekuwepo na ushirikiano usioridhisha kati ya Asasi za kiraia na Sekta Binafsi katika kutatua changamoto za kimaendeleo nje ya ushirikiano wa kiufadhili lakini sisi ni wamoja na ushirikiano kati ya sekta mbalimbali miongoni mwa mashirika, taasisi na wananchi ni moja ya hatua zinazohitajika kuchukuliwa.,” amesema Nsekela.

Ameongeza kuwa, “Katika Sekta Binafsi tunaongelea uwekezaji unaoleta matokeo chanya. Huu ni uwekezaji unaofanywa kwa lengo la kuleta matokeo ya kijamii au kimazingira yanayopimika mbali na faida za kifedha. Lengo ni kuleta maendeleo ya kijamii na uthabiti wa kiuchumi.”

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga amezungumzia kwa ufupi historia ya Wiki ya Asasi za Kiraia kwa kusema, “Ujumbe wa mwaka 2018 ulikuwa ni ‘Ukuzaji wa Viwanda Tanzania: Watu, Sera na Utekelezaji.”

Amesema, kwa mwaka 2019 ujumbe ulikuwa ni ‘Maendeleo Kupitia Ushirikiano: Ushirika Kama Chachu ya Maendeleo Tanzania’, na mwaka 2021 ni ‘Mchango wa Asasi za Kiraia kwa Maendeleo ya Taifa’ na tangu kuanzishwa kwake, kumekuwa na ongezeko la utambuzi miongoni mwa wadau katika jukwaa hilo linalowakutanisha wadau mbalimbali.

“Sisi sote ni mashahidi wa umuhimu na matokeo chanya ya Wiki ya Asasi za Kiraia tangu ilipoanzishwa, ikiwa ni pamoja na kuimarishwa kwa umoja na mshikamano miongoni mwa wadau wa maendeleo nchini,” amefafanua Henga.

Wiki ya Asasi za Kiraia, imekuwa ikileta mwamko miongoni mwa washirika wa maendeleo wa umuhimu, kwa kuionyesha jamii mchango wao juu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Wiki ya Asasi za Kiraia ya 2022 inawakutanisha washirika muhimu wa maendeleo ikiwa na lengo la kuimarisha ushirikiano utakaokuza ushiriki wa Asasi hizo katika maendeleo ya Tanzania, kuimarisha hatua za pamoja zenye lengo la kufanyia kazi changamoto za kimaendeleo na kubadilishana mawazo kuhusu changamoto.

Polisi yagundua miili 20 iliyokaushwa, watatu wakamatwa
Urusi, Ukraine zashutumiana mapigano karibu na Nyuklia