Wadau mbalimbali nchini wameishauri Serikali kufikiria namna ya kutumia lugha ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia shuleni ili kukuza na kuendeleza lugha hiyo.

Ushauri huo umetolewa Jijini Dodoma katika Mdahalo wa Kumbukizi ya Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius K. Nyerere uliofanyika katika ukumbi wa Chuo cha ST. .Jonhs of Tanzania ambapo mada mbalimbali ziliwasilishwa na kujadiliawa na washiriki.

Awali Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo. Dkt. Harrison Mwakyembe akifungua mdahalo huo amesema kuwa lugha ya Kiswahili ndio lugha kuu ya mawasiliano hapa nchini na ndio lugha inayowatambulisha watanzania Ulimwenguni.

“Kiswahili hivi sasa ni lugha kubwa sana duniani na inazungumzwa na watu wengi hivyo ni lazima watanzania wakawa mstari wa mbele kukikuza na kukiendeleza kwa kukizungumza kwa ufasaha,”amesema Dkt. Mwakyembe.

Aidha Dkt. Mwakyembe amemuagiza Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Godfrey Muingereza kuhakikisha kuwa katika mashindano yajayo ya ulimbwende washiriki wanatumia lugha ya Kiswahili katika mashindano ya ndani na watakapoiwakilisha nchi kimataifa.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Susan Mlawi ameongeza kuwa mdahalo huo ni muendelezo wa Kampeni ya Uzalendo na Utaifa inayotarajiwa kufikia kilele chake Disemba 08 mwaka huu ambapo itatanguliwa na matukio tofauti kiwemo Mijadala,makongamano na nyimbo mbalimbali na kauli mbiu mwaka huu “Kiswahili Uhai wetu,Utashi wetu.”

 

Aliyelipua bomu na kuua mamia ahukumiwa kifo
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Oktoba 15, 2018