Wafanyabiashara wakubwa kumi wa mkoani Njombe wanashikiliwa na jeshi la polisi kufuatia matukio ya kutekwa na kuuawa kwa watoto mkoani humo.

Hayo yalisemwa jana na Mbunge wa Makambako, Deo Sanga alipokuwa akichangia hoja bungeni kwenye mjadala kuhusu hali ya sintofahamu ya maujai ya watoto mkoani Njombe.

Sanga alisema kuwa hali hiyo imezua taharuki na kusababisha sintofahamu kwa wageni wanaotembelea mkoa huo kwani wengine hudhaniwa kuwa ni wezi wa watoto.

“Hali ya Njombe ni tete na imeleta taharuki kubwa sana. Na baadhi ya wageni wakifika katika maeneo mbalimbali wanahofiwa kama wamekuja kuteka watoto au kuua,” alisema Sanga.

“Na hivi sasa tunavyozungumza, baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wamekamatwa katika mji wa Makambako. Wana siku nne hivi sasa ndani na hatujui kinachoendelea,” aliongeza.

Alisema kuwa kwakuwa wafanyabiashara hao walikuwa wameajiri mamia ya watu, baadhi ya shughuli za biashara zimesimama kufuatia kukamatwa kwao.

Aidha, alisema kuwa kutokana na taharuki ya kuuawa kwa watoto, kumezuka tabia ya wananchi kutaka kuwavamia na kuwaua watu wasiowafahamu kwa madai kuwa ni wezi wa watoto. Alitoa mfano wa mwanafunzi mmoja aliyenusurika kuuawa na wananchi alipomtembelea mwanafunzi mwenzake ambaye kwa bahati mbaya hakumkuta katika nyumba aliyopanga ambayo ilikuwa na watoto pia.

Alisema baada ya wananchi kumkamata mwanafunzi huyo, walimpigia simu mwenye nyumba ambaye alieleza kutomfahamu, ndipo walipoanza kusadiki kuwa atakuwa mwizi wa watoto. Lakini mwanafunzi huyo aliokolewa na polisi na ukweli ukabainika.

Akizungumza jana mkoani Njombe, Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Renata Mzinga alikiri kuwa jeshi hilo linawashikilia baadhi ya wafanyabiashara wakubwa.

Alisema jeshi hilo limebaini mtandao wa watuhumiwa waliokuwa wakifanya vitendo hivyo na kwamba hata waliokimbia watatafutwa hadi wafikishwe kwenye mkono wa sheria.

“Tumebaini mtandao wa watu waliokuwa wanahusika na mauaji haya. Kwa kushirikiana na kikosi maalum kutoka makao makuu jijini Dar es Salaam ambacho kimeungana nasi, tutawasaka kokote walipo,” alisema Kamanda Mzinga.

“Hadi sasa tumeshakamata watu 28 ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara wakubwa, waganga wa kienyeji na wananchi wa kawaida,” aliongeza.

Spika wa Bunge, Job Ndugai ameipa muda Serikali, hadi Februari 8 mwaka huu, kuwasilisha bungeni taarifa ya kinachoendelea mkoani Njombe.

Mawaziri kulipwa mishahara na marupurupu maisha yao yote
Mfumo wa Kibubu cha Malipo ya Ada Kukomboa Wazazi Tanzania