Halmashauri ya Manispaa ya Ilala Jijini Dar es Salaaam imewataka wafanyabiashara kuzingatia muda uliopangwa na Serikali kwa ajili ya usafi wa mazingira katika maeneo yao ya kazi unaofanywa kila ifikapo siku ya jumamosi.

Muda uliowekwa kwa ajili ya zoezi hilo ni kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 3:30 asubuhi, ambapo wafanyabiashara wote watapaswa kufungua maduka na masoko yao mara baada ya zoezi hilo kukamilika.

Hayo yamesemwa leo na Afisa wa Manispaa hiyo, David Langa wakati alipokuwa akiongea na mwandishi wa habari hii kuhusu mwitikio wa wananchi juu ya zoezi la usafi wa mazingira unaofanyika kila jumamosi na kila mwisho wa mwezi.

“Nawaomba Wafanyabiashara wenye tabia ya kujichelewesha ili wafike baada ya muda wa usafi pamoja na wale wanaofungua biashara kabla ya muda uliopangwa na Serikali kuacha mara moja kwani  lengo la kubadili muda wa kufungua biashara ni kwa ajili ya kufanya usafi” alisema Langa.

Akifafanua zaidi Langa aliwatahadharisha wananchi wanaopenda kutupa taka hovyo kuacha mara moja kwani sheria ya afya na sheria ya mazingira inapinga suala hilo na kwa mujibu wa sheria hizo adhabu yake ni faini ya shilingi milioni moja au kifungo kisichozidi miaka 6.

Kwa mujibu wa Langa alisema kuwa, suala la usafi sio suala la Serikali pekee bali wananchi wanatakiwa walifanye kuwa ni sehemu ya kulinda afya zao, hivyo kila mmoja anapaswa kuzingatia usafi kwenye maeneo yanayomzunguka.

Aidha Langa alisema kila mwananchi anapaswa kuwa mlinzi wa mwenzie kwani zoezi la kulipishwa faini bado ni endelevu, mtu atakaemkamata mwenzie anatupa taka atapewa shilingi elfu 20 na aliyekamatwa atatoa faini ya shilingi elfu 70

Video: Ugonjwa wa Sumu Kuvu watajwa kuwa changamoto kubwa
Lukuvi Atatua Mgogoro Wa Ardhi Magomeni Kota