Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (NIDA) imetangaza kusitisha mikataba ya wafanyakazi wake 597 kutokana na kuwa na bajeti ndogo.

Taarifa hiyo imekuja ikiwa ni siku chache baada ya Mamlaka hiyo kukiri kuwa vitambulisho vya Taifa vilivyotumia kiasi kikubwa cha fedha za umma havikuwa na ubora unaotakiwa ikiwa ni pamoja na kukosa sahihi ya mwenye kitambulisho na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo.

“NIDA imesitisha mikataba yote ya wafanyakazi wa mkataba waliopo katika ofisi zetu zote nchini. Hii ni kutokana na mahitaji ya watumishi na bajeti, kwa hali ya sasa NIDA hatuna bajeti ya kuendelea kuwalipa wafanyakazi ambao idadi yao ni 597,” Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Dk. Modestus Kipilima alieleza kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Alisema kuwa sababu nyingine ni kubadilika kwa mpango kazi wa Mamlaka hiyo pamoja na eneo la majukumu yake kwakuwa hatua zote za usajili sasa zitafanyika katika ngazi ya wilaya na watumishi wachache watatekeleza kazi hiyo kwa kushirikiana na watendaji katika ngazi za mitaa na vijiji.

Lukuvi aahidiwa rushwa ya Bilioni 5
Chanzo cha Maalim Seif kukimbizwa hospitali ghafla chawekwa wazi