Sakata la Chama cha Wananchi CUF limeendelea kuchukua sura mpya mara baada ya wafuasi wa Prof. Ibrahim Lipumba kushikiliwa na Jeshi la Polisi akiwemo  Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chama hicho, Abdul Kambaya.

Hayo yamesemwa na Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam, Simon Sirro alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam, amesema kuwa wafuasi hao wamekamatwa kwa tuhuma za kufanya fujo kwenye mkutano wa wafuasi wa Maalim Seif.

Amesema kuwa wiki iliyopita wafuasi hao wanatuhumiwa kufanya fujo katika mkutano ulioandaliwa na Mwenyekiti wa CUF Kinondoni, Juma Nkumbi na kuwajeruhi waandishi wa habari pamoja na wafuasi wenzao wanaomuunga mkono Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif.

Aidha, katika hatua nyingine, Sirro amepiga marufuku shughuli za usafi zilizokuwa zimepangwa CUF upande wa Maalim Seif za kwenda kufanya usafi katika Ofisi za Chama hicho zilizopo Buguruni Jijini Dar es salaam.

“Kama wanahamu sana ya Kufanya usafi siku hiyo ya Jumapili, wafanye kwenye nyumba zao, mitaa na Ofisi wanazofanyia kazi na haturuhusu mtu kuingia kwenye Ofisi hizo za Buguruni,”amesema Sirro.

Hata hivyo, Mgogoro huo wa Chama cha Wananchi CUF umedumu kwa muda mrefu mara baada ya Prof. Lipumba kujiuzuru nafasi ya Uenyekiti na Baadaye kuamua kurudi kwenye nafasi yake, kitendo ambacho kilipingwa na baadhi ya wanachama ambao walihoji uhalali wa kurudi katika nafasi hiyo.

 

 

Trump Akejeli Jaribio La Kombora La Korea Kaskazini Jana, ‘Ni Dharau’
Magazeti ya Tanzania leo Aprili 29, 2017