Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amewataka wafugaji wa Mkoa wa Pwani kuanza kuvuna mifugo na kuiuza kwani kwa kufanya hivyo itasaidia kuwaongezea kipato na kupunguza migogoro kati yao na watumiaji wengine wa ardhi.

Ulega ameyasema hayo wakati akiongea na wafugaji na wakulima wa Wilaya ya Rufiji alipofanya ziara wilayani humo kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.

Amesema ni muhimu viongozi wa wilaya za Rufiji, Mkuranga na Kibiti kukaa na wadau wa mifugo kutengeneza mkakati wa kuhamasisha uvunaji wa mifugo yao kwakuwa soko la kuuza lipo mkoani humo na bado hawajalitumia ipasavyo.

“Hapa mkoa wa Pwani tuna kiwanda cha Nyama cha TanChoice lakini pamoja na kiwanda hicho kuwepo hakuna mifugo inayopelekwa pale kutoka ukanda wetu huu wa Pwani,” amesema Ulega

Amesema kuwa ili faida ya uwepo wa kiwanda hicho ionekane ni vyema wadau wote wa mifugo mkoani humo waanze uvunaji mkubwa na kupeleka kuiuza kiwandani hapo.

“Tunatamani kuona mifugo inatoka katika ukanda huu wa Pwani na kwenda kuuzwa jijini Dar es Salaam ambapo ndipo kwenye biashara kubwa ya nyama, msione fahari kukaa na makundi makubwa ya mifugo ambayo mwisho wa siku yakaonekana kuwa ni kero na hayana faida,” Naibu Ulega.

Habari Picha:Rais Mwinyi akutana na mabalozi walioteuliwa
Jaji Mutungi kukutana na vyombo vya ulinzi na usalama