Baadhi ya Waganga wa Jadi wameanza kutoroka mkoani Njombe na kukimbilia mikoa ya jirani kutokana na msako mkali wa jeshi la polisi unaoendelea mkoani humo ili kuwabaini wanaojihusisha na ramli chonganishi zinazosababisha mauaji ya watoto.

Hayo yamesemwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe, Renatha Mzinga ambapo amesema kuwa jeshi la polisi halitaweza kuwaacha wale wote waliokuwa na nia ovu na kuwatafuta popote pale walipo.

“Tunao Waganga 6 tunaowashikilia mpaka sasa kwa mahojiano na tulivyoanza na kamata kamata wale ambao wana nia ovu wamekimbia, lakini hata hivyo tunaendelea kuwafuatilia kule waliko hatutawaacha kwasababu tunaamini kabisa wao ndio waliotoa maelekezo ambayo yanaangamiza kizazi chetu hiki cha watoto wadogo”amesema Kamanda Mzinga

Aidha, amesema kuwa mpaka sasa jeshi hilo la polisi limekwisha hakiki leseni 50 za Waganga wa Jadi huku wakiendelea na zoezi hilo mpaka litakapo kamilika.

Katika hatua nyingine jeshi hilo la polisi limesema kuwa mpaka sasa linataarifa ya mtoto mmoja tu aliyepotea mwenye umri wa miaka 7 kutoka kijiji cha Ikando ambaye bado hajapatikana.

Hata hivyo, Jumla ya watu 28 wakiwemo Waganga wa jadi, Wafanyabiashara pamoja na wananchi waliojichukulia sheria mkononi na kufanya mauaji dhidi ya vijana wanaohisiwa kutekeleza mauji ya watoto wanashikiliwa na polisi kwa ajili ya upelelezi huku mpaka sasa jumla ya watoto 7 wamepoteza maisha kwa matukio ya mauaji mkoani humo.

Video: Wakili Manyama amtaka Lissu ajitathimini,'Akigoma afutiwe ubunge'
Wauguzi wagoma, huduma hospitalini zazorota

Comments

comments