MWENYEKITI wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji mstaafu Hamisa Kalombola ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), kuendelea kuwa wabunifu ili kuhakikisha majisafi na salama yanapatikana wakati wote.

Jaji Kalombola, ameyasema hayo wakati wa ziara ya kikazi ya makamishna wa tume hiyo katika ofisi za DUWASA ambapo alizungumza na menejimenti ya Mamlaka hiyo, na kuwataka watumishi kujiepusha na utovu wa nidhamu, uzembe, wizi, ubadhilifu, uombaji wa rushwa ili wananchi wapate huduma bora.

Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji Mst. Hamisa Kalombola, akizungumza na menejimenti ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) wakati wa ziara ya Makamishna wa Tume Utumishi wa Umma katika Mamlaka hiyo jijini Dodoma.

Amesema, “Mamlaka yenu iendelee kufanya tathmini ya mipango yake ili uwekezaji unaofanyika uwe na matokeo chanya na lengo la Serikali la kuwaletea watanzania ustawi wa maendeleo liweze kufikiwa hapo mtaweza kutotenda makosa kwa kuhakikisha wakati wote mnatekeleza majukumu kwa kuzingatia sheria, kanuni na utaratibu.”

Kwa upande wake, Kamishina wa Tume hiyo, Susan Mlawi amesema wao kama tume wana jukumu la kuweza kufahamu mazingira ambayo watumishi wanafanya kazi ikiwa sheria, kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma zinazingatiwa.

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph alisema kwa sasa miradi ambayo inahitajika kutekelezwa kwa uharaka ni kupeleka maji mjini Dodoma kwa kutumia bwawa la Mtera wakati ikisubiriwa maji ya Bwawa la Farkwa au ziwa Victoria ambayo yanaweza kuchukua muda mrefu.

Amesema mahitaji ya maji kwa Jiji la Dodoma ni lita milioni 133 kwa siku lakini yanayozalishwa kwa sasa ni lita milioni 67 hivyo kuna upungufu wa lita milioni 66 lakini mradi wa maji kutoka Bwawa la Mtera unatarajia kuingia lita 68 na kufanya jiji liwe na lita 201 milioni ambayo yatatosha kwa matumizi walau kwa miaka 13 ijayo.

Kenya: Odinga ataja sababu kuukubali ushindi wa Ruto
Balozi Mulamula agusia utekelezaji Diplomasia ya uchumi