Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limefanya uteuzi wa wanafunzi waliohitimu elimu ya sekondari kidato cha sita kutoka shule zote za Tanzania Bara kwa mwaka 2018 kuhudhuria mafunzo ya JKT kwa mujibu wa Sheria.

Pamoja na uteuzi huo, JKT limewapangia Makambi ya JKT watakayokwenda kupatiwa mafunzo kwa muda wa miezi mitatu na wanatakiwa kuripoti makambini hayo kuanzia June tarehe 1 hadi 10 2018.

Wahitimu wamepangiwa katika Kambi za JKT Rwamkoma – Mara, JKT Msange – Tabora, JKT Ruvu – Pwani, JKT Makutupora – Dodoma, JKT Mafinga – Iringa, JKT Mlale – Ruvuma, JKT Mgambo na JKT Maramba – Tanga, JKT Makuyuni – Arusha, JKT Bulombora, JKT Kanembwa, Nachingwea- Lindi na JKT Mtabila – Kigoma.

Aidha, wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho (physical disabilities) wanatakiwa kuripoti kambi ya Ruvu JKT iliyopo mkoani Pwani ambayo ina miundombinu ya kuhudumia jamii hiyo.

Vijana watakaochaguliwa watatakiwa kujigharamia nauli za kwenda na kurudi kwenye makambi ya JKT waliyopangiwa wakiwa na vifaa vifuatavyo: Bukta ya rangi ya Dark blue yenye mpira kiunoni (lastic), iliyo na mfuko mmoja nyuma, urefu unaoishia magotini isiyo na zipu. Aidha bukta za wanawake zinatakiwa kuwa na lastic magotini, Raba za michezo zenye rangi ya kijani, Shuka mbili za kulalia zenye rangi ya blue bahari, Soksi ndefu za rangi nyeusi, Nguo za kuzuia baridi kwa waliopangwa kwenye mikoa yenye baridi, Track Suit ya rangi ya kijani au bluu.

Mkuu wa JKT anawakaribisha vijana wote walioteuliwa ili waweze kujiunga na vijana wenzao katika kujifunza Uzalendo, Umoja wa Kitaifa, stadi za kazi, stadi za maisha na Utayari wa kulijenga na kulitumikia Taifa letu. Orodha kamili ya majina ya vijana na makambi ya JKT waliyopangiwa vinapatikana kwenye tovuti ya JKT ambayo ni www.jkt.go.tz

Kikwete atoa neno la hisia kwa Rais Magufuli, Kinana na Bashiru
Manchester City waweka kambi mjini Naples, Italia