Taasisi ya Sekta binafsi Nchini (TPSF) imetoa wito kwa wahitimu na vijana waliopo vyuoni kuchangamkia fursa ya mpango maalum uliobuniwa baina yake na Serikali ambao umekusudia kuwajengea ujuzi kabla ya kuajiriwa  ili waweze kufanya kazi kwa weledi.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye wakati alipokuwa akichangia mada kuhusu wahitimu wa vyuo vikuu kushindwa kuonyesha ujuzi baada ya kuajiriwa.

“Upo upungufu mkubwa wa mafunzo ya vitendo kwa wahitimu wengi wanaomaliza vyuo vikuu nchini na imedhihirika kuwa wahitimu hao hushindwa  kufanya kazi kwa weledi wanapokuwa wameajiriwa na Sekta mbali mbali,” amesema Simbeye.

Amesema kuwa mpango huo maalum umeanzishwa kwa lengo la kuwatayarisha  wahitimu wa vyuo kupata mafunzo ya muda mfupi ili kuondoa changamoto wanazokabiliana nazo pindi wanapoajiriwa au kutaka kujiajiri.

Simbeye ameongeza kuwa Mpango huo pia umekusudia kuwapunguzia gharama waajiri, hasa wa sekta binafsi kwa kuwa wengi wao wamekuwa wakitumia pesa nyingi kwa kuwapeleka waajiriwa wapya katika mafunzo ili waweze kumudu kazi zao.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana, na Walemavu), Anthony Mavunde amesema kuwa mpango wa Serikali ni kuhakikisha kuwa kila chuo kinajitengenezea mwongozo wake unaomwezesha kila mwanafunzi kupata nafasi ya kufanya mafunzo kwa vitendo.

Hata hivyo, ameongeza kuwa Serikali itahakikisha kuwa mpango huo unakuwa endelevu na unafanya kazi kama ilivyokusudiwa na kutoa wito kwa sekta binafsi na waajiri kutoa maoni yao ili kuboresha mpango huo

Halmashauri zote nchini zaagizwa kuwasilisha taarifa za MKURABITA
Laurent Blanc Kurithi Mikoba Ya Luis Enrique?