Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage
amewataka wahitimu 1,811 wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE)
waliotunukiwa stahili zao katika Fani mbalimbali kwa mwaka 2016
kuchangamkia fursa za ajira zilizopo nchini kwa kuanzisha makampuni na
viwanda vidogo vidogo vitakavyowawezesha kujiajiri na kuajiri wengine.

Ameyasema hayo katika mahafali ya 51 ya chuo hicho jijini Dar es salaam
, Mwijage  amesema kuwa makampuni na viwanda vidogo vidogo
watakavyoanzisha vitatumika kuzalisha bidhaa mbalimbali zenye ubora
ambazo zitauzwa kote duniani hivyo kukuza uchumi wa nchi na kuwapatia
ajira ya uhakika.

Ameongeza kuwa Serikali ya Tanzania inapenda kuwaona Wawekezaji wengi wa
Kitanzania wakiingia  na kuwekeza kwenye rasilimali mbalimbali
zilizopo nchini Tanzania badala ya kuwaachia wageni kwa kuwa inao
wasomi waliobobea kwenye fani ya biashara pamoja na  ujasiriamali.

” Taifa letu limebarikiwa kuwa na fursa nyingi za kujiletea maendeleo,
Serikali ingependa kuona wawekezaji wengi wa Kitanzania wakiwekeza
kwenye rasilimali zilizopo kwa mfano tunayo gesi, madini, kilimo na na
rasilimali nyinginezo nyingi”  Amesisitiza Mhe.Mwijage.

Amefafanua kuwa Serikali itaendelaea kuwekeza kwenye Elimu ya Biashara
kuwawezesha wananchi wengi zaidi kujiajiri na kuajiriwa katika sekta
binafsi hasa Biashara.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Prof.Emanuel
Mjema akizungumza wakati wa mahafali hayo ameeleza kuwa chuo
anachokisimamia kimeweza kutoa wahitimu kwenye mafunzo ya biashara
nyanja za Uhasibu , Usimamizi wa Biashara, Usimamizi wa Masoko ,
Ununuzi na Ugavi , Mizani na Vipimo ,TEHAMA pamoja na mafunzo ya
Shahada ya Ualimu katika Biashara.

Hata hivyo baadhi ya wahitimu wa chuo hicho waliohudhuria mahafali
hayo wakizungumza kwa nyakati mbalimbali wamesema kuwa wako tayari
kulitumikia taifa kwa kuwa wanao uwezo na ujuzi wa kutekeleza majukumu
yao kikamilifu.

Mchungaji amchapa mwandishi wa habari Arusha
Chadema wamtimua kada wao aliyegombea ubunge, wadai aliuza ushindi