Wahitimu wa mahafali ya 30 wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) wametakiwa kuwa waadilifu, wachapakazi na wazalendo kwa nchi yao, watakapokuwa wanatekeleza majukumu yao kwa ajili ya maslahi ya Taifa.

Hayo yamesemwa mkoani Mtwara na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa alipokuwa akiwatunuku vyeti wahitimu hao katika mahafali yaliyofanyika Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Kampasi ya Mtwara.

Amesema kuwa, waajiri wote nchini wanatambua umahiri wa utendaji kazi wa wahitimu wanaotoka Chuo cha Utumishi wa Umma, hivyo amewataka wahitimu hao kuendelea kujenga taswira nzuri ya chuo kwa kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na weledi.

Dkt. Mwanjelwa ameongeza kuwa, sasa ni wakati muafaka kwa wahitimu hao kuonyesha utofauti wao kiutendaji na wahitimu wengine ambao hawakupata fursa ya kusoma Chuo cha Utumishi wa Umma.

Aidha, amewahimiza wahitimu hao, kufanya kazi kwa ufanisi na kuwa wabunifu katika utendaji kazi ili kukidhi mahitaji ya wananchi na kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli ambaye anaiishi kwa vitendo kaulimbiu yake ya HAPA KAZI TU.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Charles Msonde amesema kuwa bodi ya taaluma ilipitia kwa kina taarifa za matokeo za wahitimu wote na kujiridhisha pasipo shaka yoyote kuwa, wanastahili kutunikiwa vyeti.

Naye Kaimu Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Dkt. Emmanuel Shindika amewataka wahitimu kuitumia elimu waliyoipata kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla, na amewapongeza waelekezi katika kampasi zote kwa kuwapa mafunzo bora wahitimu hao, ikiwa ni pamoja na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mchango wake katika kukiboresha chuo hicho.

Jumla ya wahitimu 2686 walitunukiwa vyeti vya awali, astashahada, stashahada na shahada ya uzamili katika fani za Utunzaji wa Kumbukumbu, Uhazili, Sheria, Menejimenti ya Rasilimaliwatu, TEHAMA, Utawala wa Umma, Manunuzi na Ugavi.

Marekani yapandisha ushuru kwa bidhaa kutoka China
Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC yaonya kuhusu taarifa za kizushi