Vijana waishio katika mazingira magumu waliohitimu Chuo cha Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Pwani, chini ya Mradi wa kuwawezesha Vijana Kiuchumi (YEE) unaoratibiwa na Shirika la Plan International wameiomba Serikali kuwapatia ajira ili waweze kumudu maisha yao.
Hayo yamesemwa leo wilayani Kibaha na mmoja wa wahitimu wa mradi huo, Rajabu Kilanga alipokuwa akiongea na waandishi wa habari  juu ya mafanikio na changamoto anazozipata baada ya kuhitimu mafunzo hayo.
Kilanga amesema kuwa mradi huo umemuwezesha kufahamu jinsi ya kuhifadhi fedha kwa ajili ya maisha ya baadaye pia umemnufaisha yeye pamoja na familia yake kwani kupitia fani ya umeme aliyoisomea ameweza kupata tenda ndogo ndogo ambazo zinamsaidia kuyaendesha maisha yake

“Pamoja na faida nyingi nilizozipata kupitia mradi huu lakini ukosefu wa ajira za kudumu ni moja ya changamoto ambazo zinatukabili vijana tuliohitimu mafunzo haya hivyo, tunaiomba Serikali itusaidie kutupatia ajira ili na sisi tuweze kutimiza malengo yetu na kuchangia katika kulijenga Taifa letu”, alisema Kilanga.
Kilanga ameishukuru EU na Shirika la Plan International pamoja na wadau wengine kwa kuratibu mradi huo kwani baada ya vijana wengi kuhitimu na kuweza kujiajiri na kupata vipato kupitia mafunzo waliyoyapata chini ya mradi huo wameweza kujikwamua kutoka kwenye hatua moja ya maendeleo kwenda nyingine.
Naye muhitimu mwingine kupitia mradi huo, Simba Musa ametoa wito kwa vijana wenzie kujituma na kufanya kazi kwa bidii kwani kwa kufanya hivyo wananchi wataona kazi zao hivyo kuwapelekea kupata ajira kwa urahisi.
“Nawashauri vijana wenzangu tujishughulishe, hata kama Mhe. Rais akitoa fedha hawezi kukuletea nyumbani kwa hiyo, kila mmoja kwa nafasi yake ajitume ili watu wazione kazi zake”, alisema Musa.
Aidha, ameyataja baadhi ya malengo yake yakiwemo ya kufungua duka la vifaa vya umeme pamoja na kuwafundisha vijana wenzie bila kuwatoza gharama yoyote ili nao waweze kujipatia kipato kupitia ujuzi watakaoupata.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Visigo, wilayani Kibaha, Aloisi Nyelo amesema kuwa mradi huo umewasaidia vijana kutozagaa hovyo mitaani kwani wameunda vikundi vinavyosimamiwa na watendaji wa Kata hiyo kwa ajili ya kuwapa ushauri hivyo kuwafanya wawe na adabu na heshima.
Nyelo ameongeza kuwa Kata hiyo iko mstari wa mbele katika kuwasaidia vijana kupata tenda mbalimbali kwa kuwabandikia matangazo nje ya ofisi zao na kuwataka wananchi wanaohitaji wafanyakazi kusaini mkataba na vijana husika mbele ya Afisa Mtendaji ili kuhakikisha wanafanya kazi kwa uhakika na wanalipwa fedha zao kama walivyokubaliana.
Mtendaji huyo alitumia fursa hiyo kutoa rai kwa wananchi kuwaamini na kuwasaidia vijana hao kwa kuwapa tenda mbalimbali zinazolingana na fani walizosomea kwani wana ujuzi wa kutosha kufanya kazi hizo katika kiwango kinachotakiwa.

Ronaldinho Gaucho Kuachana Na Soka
Azam V Simba Sept. 17 Uwanja Wa Uhuru, Azam Yapewa Ngao