Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki ameagiza maafisa mifugo na madaktari wa mifugo, Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu, walioandika au kushuhudia vyeti vya vifo vya ng’ombe zaidi ya 270 ambao walikamatwa na uongozi wa Pori la Hifadhi la Maswa kusakwa na kufikishwa katika Baraza la Veterinari Tanzania ili kuchunguzwa.

Aidha, Waziri Ndaki amewaagiza wakuu wa Wilaya za Itilima na Meatu kufikia Siku ya Jumanne (21.09.2021) wawe wamefikisha taarifa rasmi wizarani juu ya idadi ya mifugo iliyokuwa imekamatwa na kurejeshwa kwa wafugaji, idadi ambayo haijarudishwa pamoja na majina ya wafugaji ambao wanadai mifugo yao baada ya kushinda kesi mahakamani kwa madai kuwa mifugo yao iliingia katika Pori la Hifadhi la Maswa.

Waziri Ndaki ameyasema hayo wakati wa ziara yake katika Wilaya za Itilima na Meatu ambapo akiwa katika Wilaya ya Itilima aliarifiwa baadhi ya wafugaji walioshinda kesi Mahakama ya Rufaa mwaka 2019, baada ya ng’ombe wao kudaiwa kuingia katika Pori la Hifadhi la Maswa mwaka 2017, kurejeshewa ng’ombe 51 pekee huku uongozi wa pori hilo ukiwaarifu ng’ombe zaidi ya 270 walikufa,

Hata hivyo wafugaji hao hawakushuhudia mizoga ya ng’ombe hao wala vyeti vya vifo ambavyo inaelezwa viliandikwa na maafisa mifugo ambao pia hawakushudia mizoga hiyo

Aidha Waziri Ndaki amewaonya maafisa mifugo na madaktari watakaobainika kuendelea kufanya kazi bila kufuata taratibu za kazi zao Baraza la Veterinari Tanzania halitasita kufuta usajili wao.

Ameongeza kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa sasa inafuatilia taarifa za wafugaji kote nchini, ambao mifugo yao ilikamatwa na baadaye wafugaji hao kushinda kesi lakini mifugo hiyo haijareshwa kwao wala fedha walizolipishwa faini, kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kutaka taarifa hiyo ambayo wizara inakusanya ili kuifikisha kwa Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa kwa ajili ya maamuzi zaidi.

“Maafisa mifugo na madaktari wa mifugo nchi nzima mnapaswa kujua nyie ni madaktari wa mifugo siyo kukaa kwenye meza na kuandika vyeti vya vifo vya ng’ombe bila kushuhudia vifo hivyo, baadhi yenu wanafanya kazi kiholela,” Amesema Waziri Ndaki

“Hili jambo siyo dogo ni kubwa nimeagizwa na Rais nije kufuatilia masuala haya watu wameshinda kesi lakini ng’ombe hawajarudishwa kwa wenyewe, nimeambiwa nifuatilie nipeleke orodha yote kwa waziri mkuu ili taarifa itolewe.” Amefafanua Waziri Ndaki.

Katika hatua nyingine wafugaji wamemuomba Waziri Ndaki kuwa, serikali iangalie namna ya kuwaruhusu wafugaji kuvuna malisho katika maeneo ya hifadhi badala ya malisho hayo kuchomwa moto ili wafugaji wawe wanayavuna na kuyatunza kwa ajili ya mifugo yao.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki amewahimiza wafugaji kuiwekea mifugo yao hereni za kieletroniki ambazo zinatambua mfugo ulipo kuanzia ngazi ya taifa hadi kijiji hali ambayo itasaidia kuzuia wizi na upotevu wa mifugo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki , (aliyejifunga shuka) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Itilima Mhe. Faiza Sileiman, wakati alipokuwa akiwasili katika vijiji vya Shishani na Lungalumbogo vilivyopo Kata ya Migato na kupokelewa na wafugaji wa kabila la kisukuma waliokuwa wakiimba moja ya nyimbo za kabila hilo kwa ajili ya mapokezi ya Waziri Ndaki alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja Mkoani Simiyu kufuatilia taarifa ya wafugaji ambao hawajarejeshewa mifugo yao licha ya kushinda kesi mahakamani kwa madai ya kuingiza mifugo katika Pori la Hifadhi la Maswa
 Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) (kulia), akibadilisha mawazo na Bw. Praisegod Zakaria Afisa Sheria kutoka Bodi ya Nyama nchini (anayemfuata), Dkt. Benezeth Lutege Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Udhibiti wa Magonjwa yaenezwayo na Wadudu pamoja na Bw. Shigi Magese Afisa Sheria kutoka wizarani. Waziri Ndaki aliwasili katika vijiji vya Shishani na Lungalumbogo vilivyopo Kata ya Migato Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku moja mkoani humo kufuatilia taarifa ya wafugaji ambao hawajarejeshewa mifugo yao licha ya kushinda kesi mahakamani kwa madai ya kuingiza mifugo katika Pori la Hifadhi la Maswa.

Hassan Dalali aishukuru Young Africans
Sita wafariki kwa ajali Ruvuma