Mbunge wa Jimbo la Ukonga kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Mwita Waitara amesema kuwa kuna baadhi ya mawakala wa Chadema walimpigia kura na kumhakikishia kuwa wanamuunga mkono.

Ameyasema hayo Jijini Dar es salaam mara baada ya kutangazwa mshindi wa kiti cha Ubunge katika uchaguzi mdogo uliofanyika jimbo la Ukonga.

Waitara amesema kuwa ushindi umepatikana na kilichobaki kwasasa ni kuchapa kazi na kuendelea kutatua kero za wananchi wa jimbo hilo.

Aidha, uchaguzi wa marudio unatokana na mbunge huyo kukihama chama chake cha awali ambacho ni Chadema na kujiunga CCM ambako aliteuliwa kugombea tena kiti hicho cha Ubunge.

“Kwanza kabisa nimshukuru Mungu na wana CCM wote walioniunga mkono na wale ambao sio wana CCM, sasa hapa ni kazi tu, lakini niwape angalizo Chadema, kama wanataka Chama chao kisife basi waachane na Mbowe, na kama wanataka chama kife waendelee kumkumbatia Mbowe,”amesema Waitara

Hata hivyo, Waitara amewaahidi ushirikiano wa kutosha wananchi wa jimbo la Ukonga, huku akisema kuwa atashirikiana bega kwa bega na viongozi ili kuweza kutatua kero mbalimbali.

 

RC Hapi awataka Maafisa Kilimo kujitathmini mkoani Iringa
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Septemba 18, 2018