Mgombea ubunge wa jimbo la Ukonga kwa tiketi ya Chadema, Asia Msangi ameonesha kushangazwa na kitendo cha mpinzani wake, Mwita Waitara kuondoka kwenye kipindi cha redio kilichoandaliwa kwa ajili yao, baada ya kumuona yeye.

Waitara ambaye alikuwa mbunge wa jimbo hilo kabla ya kuhama Chadema na kujiunga na CCM, alifika katika kituo cha East Africa Radio kwa ajili ya kushiriki katika kipindi cha asubuhi lakini kwa mujibu wa mtangazaji wa kipindi hicho, alighaili baada ya kumuona Asia akiwa sehemu ya kipindi hicho pia.

Katika mahojiano ambayo aliendelea kufanya Asia bila Waitara, mgombea huyo alieleza mambo ambayo amepanga kuyafanya endapo atachaguliwa kuwa mbunge, huku akijiepusha na suala la kumzungumzia mpinzani wake hadi alipolazimika kwa kubanwa na maswali.

“Huyo Waitara kama alifanya hayo wakati akiwa mbunge ni yeye, lakini mimi bado naona kuna mambo mengi nikitembea wananchi wa Ukonga wanayalalamikia na nataka nikayajengee hoja na kwa kutumia vyanzo vingine vya wafadhili ambao ni rafiki zangu naamini tutayatatua,” alisema Asia.

“Ndugu mtangazaji, mimi sitaki kumzungumzia mtu hapa. Huyo Waitara kama angetaka angekuja hapa, mbona [aliponiona] amekimbia?” Alihoji.

Mgombea ubunge jimbo la Ukonga, Mwita Waitara (CCM)

Mtangazaji wa kipindi hicho alieleza kuwa Waitara ambaye alifika kwenye kipindi hicho, alighaili baada ya kumuona Asia akieleza kuwa hataweza tena kushiriki kipindi hicho hadi aombe kibali kwenye chama chake, na kwamba kuna utaratibu wa kufuata.

Asia ambaye ni Mwenyekiti wa umoja wa wanawake wa Chadema jimbo la Ukonga, amesema kuwa ingawa Waitara aliweza kutekeleza baadhi ya mambo kama ujenzi wa daraja la Kivule, yeye ameweza kufanya kazi nyingi na wananchi wa Ukonga hata kabla hajawa mbunge hivyo akiwa mbunge atafanya zaidi.

“Nimekuwa nikishirikiana na wananchi wa Ukonga kuanzia wanawake kwa kuwasaidia kupata mikopo kwenye mabenki na kuwapa elimu ya ujasiliamali. Vijana kwenye michezo, na hata nilikuwa nahudhuria vikao vya umoja wa wazee ili kushirikiana kutatua changamoto,” alisema.

Akizungumzia kuhusu matarajio yake katika uchaguzi huo, alisema anaamini kuwa atashinda lakini yuko tayari kukubali matokeo ya kushindwa kama yatakuwa ya haki.

Aliyerudisha Musoma Hotel kwa Serikali apewa kibano kingine
Wadau wa Elimu wazidi kutoa maoni