Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, amewataka Wakala wa Barabara (TANROADS), kukutana na wadau wa usafirishaji mara kwa mara ili kuwaelimisha Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018  zinavyofanya kazi ili kuondoa malalamiko ya mara kwa mara.

Akikagua utendaji kazi wa Mizani ya Nala jijini Dodoma leo September 10, Naibu Waziri Waitara amewataka wafanyakazi wa mizani kutoa elimu kwa kila dereva wa lori kila anapokaguliwa ili kuepusha madereva hao kuongeza mizigo njiani na kusababisha usumbufu kwa wamiliki wa malori na lawama kwa wafanyakazi wa mizani.

“Hakikisheni mnapopima magari mnawaeleza uzito uliopo na ni nini anastahili dereva kufanya ili kuepuka kuzidisha uzito na kuharibu barabara”, amesisitiza Naibu Waziri huyo.

Akiwa katika mizani hiyo Naibu Waziri Waitara, ameshuhudia baadhi ya madereva wa malori kukiri kuongeza mizigo ya ziada na hivyo kukamatwa kutokana na kuzidisha uzito hali ambayo inasababisha usumbufu kwa wamiliki.

Aidha amewataka wasimamizi wa mizani kote nchini kuhakikisha kwamba abiria wa mabasi yaliyozidisha uzito hawapati usumbufu wanapokuwa safarini kwa makosa ya madereva.

Pia amewasisitiza watumishi wa mizani kuhusu umuhimu wa kutenda haki kwa magari yote yanayozidisha uzito ili kuondoa malalamiko na upendeleo.

Naye, Kaimu Meneja wa TANROADS, Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Salehe Juma, amesema magari mengi yanayotozwa faini yanatokana na ukaidi wa madereva wenyewe kutotoa taarifa kwa wamiliki pindi wanapokamatwa kwa kosa la kuzidisha uzito kwani sheria inatoa fursa kwa magari kukaa siku tatu bila ya kuchajiwa kwa ajili ya kupunguza mizigo iliyozidi.

Naibu Waziri huyo yuko kwenye ziara ya kukagua changamoto zinazoikabili Kitengo cha Mizani ikiwa ni muendelezo wa mkakati wa Wizara kujenga taswira njema katika huduma ya usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya nchi.

Moto wateketeza gereza, wafungwa wapoteza maisha
Rais Samia afanya uteuzi