Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mwita Waitara amewashauri wananchi kuchagua viongozi wenye kipato katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Dar24 leo, Septemba 12, 2019 bungeni jijini Dodoma, Waitara amesema kuwa uwenyekiti wa mtaa ni kazi ya kujitolea, hivyo anayechaguliwa ni vyema akawa na njia mbadala ya kujipatia kipato na sio kutegemea nafasi atakayochaguliwa.

Ameeleza kuwa endapo mtu asiye na kipato ataiona nafasi hiyo kama fursa ya kazi na kufanikiwa kuchaguliwa kuna hatari ya kuigeuza ofisi yake kuwa kitegauchumi akiuza mihuri na kutafuta fedha kwa kuuza mihuri na ardhi ya umma.

“Sifa mojawapo ya Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa au Kitongoji ni lazima awe na kipato. Kazi ya Mwenyekiti wa Mtaa, Kijiji au Kitongoji ni kazi ya kujitolea na sio kazi ya masaa yote. Ni kazi ya siku mbili tu labda uende pale ofisini usikilize hoja mbalimbali na utambulisho,” Waitara ameiambia Dar24.

“Kwahiyo, hatutarajii mtu ambaye hana kazi anaona kama ni fursa… mkishamchagua mtu ambaye hana kipato na hana malengo na nyie, mwisho wa siku itakuwa ni migogoro, dhuruma kwa wananchi, wanauza viwanja, mnauziwa na mihuri na likitokea jambo dogo tu la kusaidia ni lazima ulipie gharama… msaada unakuwa haupo,” ameongeza.

Katika hatua nyingine, Waitara amefafanua kile alichokieleza kuwa ni taarifa aliyoisoma kwenye gazeti moja la kila siku kwamba ili mtu ashiriki kupiga kura katika uchaguzi huu wa Serikali za Mitaa anapaswa kuwa na vitambulisho takribani nane.

Angalia video hapa kuona mahojiano yote ya Dar24 na Naibu Waziri, Mwita Waitara ambaye pia ni Mbunge wa Ukonga.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Septemba 13, 2019
Neema yaendelea kudhihiri TFF, yasaini mkataba ya mabilioni