Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais muungano na mazingira, Mwita Waitara amesema utendaji kazi wa aliyekuwa Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli ndio sababu ya kuhamia CCM akitokea Chadema ili kuunga mkono juhudi za kiongozi huyo.

Amesema hayo leo machi 25, 2021, katika uwanja wa Magufuli wilayani Chato wakati wa shughuli ya kumuaga Hayati Magufuli.

Amesema kuwa utendaji kazi wa Dkt. Magufuli uliua sera na hoja za upinzani na aliona ni wakati wa kujiunga na CCM kwa kuwa mengi yalitekelezwa.

Mwita aliyekuwa CCM kabla ya kujiunga Chadema alirejea kwenye chama hicho tawala Julai 2018 na baadaye CCM kilimpitisha kuwania ubunge katika jimbo la Ukonga na kuibuka mshindi.

“Huu ni miongoni mwa misiba iliyowahi kunigusa sana, aliyeniteua kwa kushirikiana na wasaidizi wake ameniamini mara mbili nikafanya naye kazi, baada ya uchaguzi akanichagua tena ni kama vile umeenda shule unasoma na kisha ukapata msiba wa anayekulipia ada lazima uumie,” amesema Waitara.

Amesema wakati msiba huo ukitangazwa alikuwa Zanzibar na ilimchukua muda kuamini kutokana na mshtuko alioupata.

Waitara amesema Magufuli alikuwa na dhamana kiutendaji na kifo chake kinawaliza wengi hasa wananchi wa kawaida.

‘Try Again’: Tunahitaji alama zote tatu
Mamia washiriki mazishi ya ndugu wanaodaiwa kufariki kwa kukanyagwa