Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo amewataka wajasiliamali wa Wilaya ya Nkasi kuhakikisha fedha za mkopo walizopewa na halmashauri hawazitumii katika matumizi binafsi bali wazielekeze katika biashara ili ziweze kuwapatia faida na kuwainua kiuchumi na hatimae kupata fedha za kujikimu kimaisha.

Ameyasema hayo alipokuwa akikabidhi mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 53 ikiwa ni asilimia 10 ya fedha za mapato ya ndani ya halmashauri kwa vikundi 15 vya halmashauri ya wilaya ya Nkasi ikiwa ni utekelezaji wa kisheria chini ya Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) lililoanzishwa Mwaka 2005 chini ya sheria na 16 ya mwaka 2004 yenye adhima ya kuwainua wananchi kiuchumi ili kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

“Kwenye vikundi vyenu mna malengo mahususi na ili haya malengo mahususi yaweze kutimia kwenye biashara hakuna kingine zaidi ya kuwa bahili lazima muwe mabahili, lazima muwe watu ambao hamkubali kutoa fedha hovyo hovyo, uskibali kutoa fedha ambayo haina mpango, leo unaambiwa kuna msiba pale wewe unachukua fedha ya mkopo unapeleka, huu sio ubahili, weka fedha yako vizuri, kama kuna shida tafuta hela nyingine,na ukichukua fedha inayotokana na hapo labda ni faida,”amesema Wangabo

Mbunge wa jimbo la Nkasi Kaskazini, Ally Kessy alisema kuwa pesa hizo ni kodi za wananchi ambazo halmashauri inapita kuzikusanya nahatimae asilimia 10 ya mapato hayo kuyagawa kama mikopo kwa wajasiliamali wanawake, vijana na walemavu na kusisitiza kuwa fedha hiyo irudishwa kadiri inavyotakiwa.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Emanuel Sekwao amesema kuwa Kwa mwaka wa fedha 2018/2019 Jumla ya vikundi 15 viliomba mikopo ya Tshs. 68,292,000.00. lakini baada ya Kamati ya Mikopo kukaa na kupitia maombi ya mikopo jumla ya kiasi cha Tshs 53,000,000 kiliidhinishwa.

Naye mkuu wa wilaya hiyo, Said Mtanda amemuhakikishia mkuu wa mkoa kuwa watajitahidi kuhakikisha wanakusanya mapato ya halmashauri kwa asilimia 100 na kutoa mikopo hiyo kwa vijana na kuwapa fursa ya kujiajiri lakini pia kuongeza viwanda vidogovidogo kutokana na shughuli mbalimbali za uzalishaji wanazojihusisha nazo wajasiliamali hao.

 

Acacia kulipa fidia wananchi zaidi ya 200
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Machi 5, 2019