Watu kumi na watatu wakiwemo wajawazito na watoto wamekufa maji wakijaribu kutoroka machafuko nchini kwao kwa kuvuka bahari ya Mediterranean kuelekea Ulaya.

Kikosi cha uokoaji cha Uhispania kinachofahamika kama ‘Poractiva Open Arms’ kimesema kimefanikiwa kuwaokoa watu 164 baada ya boti waliyokuwa wamepanda kuzidiwa na uzito wa abiria na mizigo na kuzama karibu na eneo la pwani ya Libya.

Picha za kusikitisha zinazoonesha miili ya wajawazito na watoto zimetumiwa na kikosi hicho kwa njia maalum kwa lengo la kuwataka ndugu na jamaa wawatambue.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, zaidi ya watu 2,200 wameripotiwa kufa maji mwaka huu wakijaribu kukatiza bahari ya Mediterranean. Hii ni sawa na wastani wa watu kumi kufa maji kila siku katika safari hizo.

Hivi karibuni, makumi ya watu walipoteza maisha katika pwani ya Sabratha nchini Libya baada ya boti waliyokuwa wakisafiria kuzama. Abiria hao walitoka eneo la ukanda wa jangwa la Sahara.

Umoja wa Ulaya umeongeza muda wa vikosi vyake vya maji kudhibiti uhamiaji haramu kupitia bahari ya Mediterranean hadi mwaka 2018 ambapo imeviongezea vikosi hivyo jukumu la kupambana na biashara haramu ya mafuta kupitia bahari hiyo.

Mwanafunzi akamatwa kwa kumkashifu Rais kwenye Facebook
Magazeti ya Tanzania leo Julai27, 2017