Baadhi ya wajumbe wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) wamejitokeza leo kupinga marudio ya uchaguzi yaliyotangazwa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jecha Salum Jecha.

Wakiongea na waandishi wa habari , wajumbe hao wameeleza kuwa marudio ya uchaguzi huo ni batili na yanaenda kinyume na katiba na sheria za Zanzibar.

“Uchaguzi wa Oktoba 25 huo haufutiki, ule ni uchaguzi utakaoendelea kubakia kwa sababu utaratibu wa kuufuta haupo katika katiba hii wala katika sheria hii,” alisema Ayoub Kabari, mjumbe wa ZEC.

“In fact, Katiba hii inatulazimu Tume lazima tumalize uchaguzi wakati fulani uliowekwa maalum ambao ni siku tatu baada ya kupiga kura… ni lazima tumalize kura na matokeo yatangazwe,” aliongeza.

Kwa upande wake Nassor Mohammed, alieleza kuwa kiasi cha shilingi bilioni 7 kilichotengwa kwa ajili ya kugharamia uchaguzi huo wa marudio ni matumizi mabaya ya fedha za umma. Pia, alidai kuwa marudio hayo yamesababisha Tume hiyo kulazimisha kufanya manunuzi kwa njia ya dharura wakati hakukuwa na dharura.

Akieleza kwanini hawajajiuzulu nafasi zao kama wanapingana na maamuzi yaliyotangazwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mohammed alisema, “Katika jambo ambalo linakwenda kinyume cha katiba na sheria, inabidi tuwepo angalau kuendelea kuwaelekeza wenzetu njia zipi sahihi za kufuatwa. Na ndio maana tumekaa kimya kwa muda mrefu, na leo tumejitokeza kuwaambieni kwamba Mwenyekiti ana maamuzi kutoka sehemu ambayo sisi hatufahamu na anayalazmisha yawe maamuzi ya Tume.”

Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salum Jecha aliitangaza Machi 20 mwaka huu kuwa tarehe ya marudio ya uchaguzi wa Zanzibar.

Hata hivyo, wakati Chama Cha Mapinduzi kikiunga mkono uamuzi huo, Chama Cha Wananchi (CUF) kimetangaza kutoshiriki marudio ya uchaguzi huo.

 

Picha: Angelina Jolie ‘Akwanguliwa’ Tena Mgongoni Akiandaa Filamu Mpya
Mazombi yadaiwa kushambulia na kujeruhi watu hovyo Zanzibar, Polisi wanena