Ripoti ya Umoja wa Mataifa, iliyozinduliwa na Tume ya Wataalamu wa Haki za Kibinadamu nchini Ethiopia imesema Jeshi la Ulinzi la Taifa la nchi hiyo na wapiganaji wa mbele wa ukombozi wa watu wa Tigray, walifanya ukiukaji sawa na uhalifu wa kivita chini ya sheria ya kimataifa inayosimamia migogoro isiyo ya kimataifa.

Ripoti hiyo ambayo ilitolewa mapema wiki hii, inadai mamlaka ya Shirikisho la nchi ya Ethiopia ilitumia njaa kama njia ya kufanikisha vita, madai ambayo yanakanushwa vikali na Mwakilishi wa kudumu wa Ethiopia katika Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Zenebe Kebede Korcho.

Korcho amesema, “Ripoti yenyewe inajipinga na inaegemea upande mmoja, na sababu kuu ni kuwa haizingatii ukatili wowote unaofanywa katika mikoa ya Afar na Amhara, lakini inaangazia Tigray pekee sasa hatuwezi kuwa na ripoti ya namna hii isiyo na usawa ni lazima kufanya mambo kwa umakini na uhakika.”

Baada ya takriban miaka miwili ya vita huko Tigray, mamilioni ya watu wanakosa chakula na bidhaa za kimsingi kaskazini mwa Ethiopia zimeadimika ambapo Korcho anadai “Chanzo pekee cha ripoti hiyoni Jeshi pekee na waliandika katika ripoti yao kile kilichoamriwa na Jeshi lakini hakuna ushahidi hata mmoja unaoonyesha serikali ya Ethiopia ilitumia misaada ya kibinadamu kama chambo cha vita.”

Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa, walifanya mahojiano huku mashahidi wakizungumzia uhalifu ulioripotiwa ikiwa ni pamoja na uporaji, mauaji na ubakaji na tume inasema ilikutana na maafisa wa Serikali ya Shirikisho, taasisi zinazohusiana, mashirika ya kimataifa, wataalam wa kitaaluma, na washikadau wengine mjini Addis Ababa.

Hadi wakati wa kuwasilishwa kwa ripoti hiyo, Serikali za Sudan na Djibouti hazikuwa zimeipa Tume fursa ya kuwahoji wakimbizi wa Ethiopia ndani ya mipaka yao na mapigano kati ya vikosi vya serikali, washirika wao na waasi wakiongozwa na Jeshi yalitawala mwezi Agosti baada ya utulivu wa miezi mitano.

Kijana Mtanzania aula UN kusongesha SGDs
Ruto atoa wito msamaha wa madeni WB na IMF