Serikali imesema haitasita kuchukua hatua za kinidhamu kwa wakaguzi wa ndani watakaoshindwa kukagua miradi ya maendeleo iliyokatika maeneo yao kwa wakati kuanzia ngazi ya Halmashauri hadi Wizarani na kwamba atakayezembea atawajibishwa.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba wakati akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika tarafa ya Ndago Wilayani Iramba mkoani Singida.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba.

Amesema Mkaguzi wa Halmashauri za Wilaya hadi Wizara ambaye atasubiri miradi ikamilike kwenye eneo lake bila kufanyiwa ukaguzi na kusababisha makosa kubainishwa na mkaguzi wa nje kutoka makao makuu katika hatua za mwisho za mradi, atakuwa amejifukuzisha kazi.

“Eneo lolote ambalo miradi inaendelea kutekelezwa, nitaongea na wenyeviti wa Halmashauri na wabunge wote na mkaguzi wa nje akikuta eneo la mradi analoenda kukagua na mkaguzi wa ndani hajakagua, mkaguzi wa eneo lile atakuwa amejifukuzisha kazi mwenyewe”, ameongeza Mwigulu.

Sehemu ya Wananchi wa Kijiji cha Ndago Wilayani Iramba, Singida, waliokuwa wakimsikiliza Mbunge wa Iramba Magharibi, Dkt. Mwigulu Nchemba.

Hata hivyo, Waziri Mwigulu ameongeza kuwa, kumejengeka utaratibu kwa baadhi ya watumishi wa umma wakiisha ajiriwa wanafaidi mshahara na hawezi kufanya kazi bila posho licha ya kuwa maeneo ya ukaguzi yapo kwenye maeneo yao ya kazi na wameajiriwa kwa kazi hizo.

Aidha amefafanua kuwa yapo maeneo yenye wahandisi zaidi ya watatu na wanalipwa mishahara kila mwezi bila kufanya ukaguzi wa miradi na matokeo yake wananchi wanajitoleaa kujenga majengo ili watoto waende shule bila kupata ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wataalamu hao kitendo ambacho hakikubaliki.

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Decemba 5, 2022
Waliokuwa mateka wakutanishwa na familia zao