Kiungo kutoka nchini Ivory Coast Yaya Toure, amemtaka wakala wake Dimitri Seluk kuzika tofauti zilizopo kati yake na meneja wa Man City Pep Guardiola.

Seluk na Guardiola walitibuana hadharani miezi mitatu iliyopita kutokana na suala la Yaya Toure, kushindwa kuchezeshwa katika kikosi cha kwanza tangu meneja huyo kutoka nchini Hispania alipotua Etihad Stadium.

Toure aliachwa katika kikosi cha Man City kilichosajiliwa kwenye shirikisho la soka barani Ulaya UEFA kwa ajili ya msimu huu, jambo ambalo liliendelea kukoleza uhasama wa Seluk na Guardiola.

Hata hivyo Seluk amethibitisha kukaa chini na Toure na kuzungumzia suala la kumaliza tofauti zilizopo dhidi ya Guardiola, huku mzigo ulio mbele yake ni kuomba radhi kwa matamshi aliyoyazungumza hadharani kuhusu meneja huyo.

“Nimezungumza na Yaya siku chache zilizopita na ameniomba kumaliza matatizo yaliopo dhidi ya Pep,” Seluk aliliambia gazeti la Daily Mirror.

“Nimekubaliana na ombi la Yaya, na nimedhamiria kufanya kila linalowezekana ili kuangalia uwezekano wa kukutana na Pep na kumaliza tofauti zilizopo kati yetu, ili kumpa nafasi mchezaji huyu kucheza soka.

“Baadhi ya mashabiki wa Man City wamekua chachu ya kusakwa kwa suluhu hii, walimfuta Yaya na kumuomba aje kwangu ili kuangalia uwezekano wa kumaliza matatizo yaliopo, ninawashukuru sana kwa jitihada zao na mimi nimeona kuna umuhimu wa kufanya hivyo.”

Pep Guardiola aliapa kutomchezesha Toure katika kikosi chake hadi hapo atakapoombwa radhi na wakala wa mchezaji huyo, kutokana na maneno aliyoyazungumza katika vyombo vya habari kwa kumtuhumu.

Piero Ausilio: Tulifanya Makosa Kumuajiri Frank de Boer
Mipango Ya Mourinho Yamkataa Schweinsteiger