Polisi Mkoani Pwani wanawashikilia watu wanne waliokamatwa ndani ya Mkoa huo wakituhumiwa kutumia mitandao ya kijamii kueneza uvumi wa vifo vya watu wakidai wamekufa kwa Corona na kutia hofu Wananchi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Wankyo Nyigea amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Frank Nyange (47), Mozes Mgao (34) Mohamedi Lutambi (47) na Bumija Senkondo (55).

“Watuhumiwa hawa wanne tuliowakamata na wengine ambao tunaendelea kuwatafuta wanasambaza taarifa za uvumi za vifo vya Watu wakidai wamekufa kwa Corona na pia wanapendekeza majina ya Viongozi wa Serikali ambao walitamani wafe haraka kwa Corona,” amesema Kamanda Nyigesa.

“Watuhumiwa hawa wanne tunaowashikilia Frank Nyange na wenzake, pamoja na wengine ambao tunawatafuta, licha ya kueneza uvumi wa vifo vya Watu wakidai wamekufa kwa Corona, pia wanatia hofu Mitandaoni kwa kudai Watanzania walio wengi watakufa kwasababu Serikali haichukui tahadhari dhidi ya wananchi wake,” ameongeza Kamanda Nyigesa.

Aidha, Jeshi la polisi Mkoa wa Pwani limetoa rai kwa Wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya Corona kwa kufuata maelekezo ya Wataalamu wa Afya na kujiepusha na matumizi mabaya ya mitandao ikiwemo kutoa taarifa za uvumi kuhusu vifo vya watu, ambazo zinatia hofu wananchi wengi, na kuahidi kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa kwa watakaofanya hivyo.

PICHA: Maandalizi dhidi ya Al Ahly yakamilika
Samia afungua Mkutano wa Kimataifa wa uwekezaji