Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias John Kwandikwa amewataka wakazi wa mikoa ya Mwanza na Geita kuchangamkia fursa za kiuchumi na kijamii zitakazojitokeza wakati wa ujenzi wa daraja litakalounganisha eneo la Kigongo na Busisi Mkoani Mwanza.

Amesema kuwa maandalizi kwaajili ya ujenzi wa daraja hilo la aina yake hapa nchini yako katika hatua ya usanifu wa kina hivyo ujenzi wake utaanza mara baada ya mkandarasi wake kutangazwa na linatarajiwa kuwa na urefu wa kilomita 3.2, litakapokamilika.

“Hakikisheni mnatoa ushirikiano kwa mkandarasi ili kazi ya ujenzi iwe nyepesi na wale watakaopata fursa za ajira fanyeni kazi kwa weledi, bidii na nidhamu,” amesema Kwandikwa.

Amesema kuwa Serikali inatumia fedha nyingi katika miradi ya maendeleo ya muda mrefu hivyo ni jukumu la wananchi kujiandaa na kubaini fursa za kiuchumi na kijamii na kuzitumia.

Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Mwanza Mhandisi Marwa Rubirya amesema kuwa daraja hilo litakuwa na njia nne  za kupitisha magari, njia ya waenda kwa miguu ambapo pia litakuwa na kina kitakachoruhusu meli kupita chini ya daraja hilo.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kwandikwa amekagua kivuko cha Kigongo-Busisi na kuagiza Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA), kuhakikisha elimu inatolewa kwa wananchi kuhusu usalama na matumizi sahihi ya utumiaji wa vivuko.

Kwa upande mkuu wa kivuko cha Kigongo –Busisi Mhandisi Abdala Atiki amesema kivuko hicho kwa sasa kinahudumiwa na Mv- Mwanza na Mv- Misungwi ambapo zaidi ya abiria elfu sita na mia tano huvushwa kwa siku.

 

Masau Bwire ajipa faraja baada ya kichapo cha Azam FC
Trump amkingia kifua Mwanamfalme, apingana vikali na CIA