Wito umetolewa kwa wakazi wa Makete waishio Jijini Dar es Salaam, kuanzisha Kampuni ya Uwekezaji na Mfuko wa Maendeleo wa Wilaya hiyo utakaoangalia fursa za kiuchumi zinazopatikana Makete, Mkoani Njombe, ili kukuza pato lao na Taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Geoffrey Mwambe, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Wanachama wa Chama cha Maendeleo Makete (MDA).

Amesema kuwa fursa ya kuanzisha kampuni na mfuko utawawezesha wakazi hao kununua hisa na umiliki pamoja na kuwapa fursa za kutafuta masoko ya bidhaa na huduma zitakazotolewa ikiwa ni sehemu ya kuitangaza Wilaya hiyo kwa wawekezaji wengine.

“Makete mna fursa nyingi za uwekezaji, kuna kilimo cha ngano, pareto, viazi, matunda na mbogamboga, pia mnayo madini mbalimbali, mnao utalii wa ndege na maua kule kwenye hifadhi ya Kituro, ndugu zangu, uwekezaji katika sekta hizo inawezekana kabisa, pia mnayo ardhi ya kutosha, ni muhimu muwekeze nyumbani” alisema Mwambe.

Mwambe amewataka wakazi hao kushirikiana na kuongeza nguvu katika kutangaza fursa na vivutio vya utalii vilivyopo katika Wilaya hiyo ambayo imebarikiwa kuwa na hali nzuri ya hewa ya kuweza kuzalisha mazao mbalimbali ya chakula na biashara.

Aidha ameongeza kuwa Wilaya hiyo inao uwezo mkubwa wa kuzalisha ngano lakini bidhaa hiyo kwa asilimia kubwa inaagizwa kutoka nje ya nchi na kuwataka ikutafakari hilo ili kuzalisha ngano
kwa wingi.

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Makete, Burton Sinene amesema kwa sasa Wilaya hiyo inahitaji wawekezaji katika kiwanda cha kutengeneza njiti za meno (bamboo toothpick) kutokana na kuwepo kwa zao la mianzi, bidhaa ambayo kwa kiwango kikubwa inaagizwa nje ya nchi kwa ajili ya matumizi ya mezani wakati wa kula.

Katika majadiliano ya kikao hicho wakazi hao waliiomba Serikali izidi kuimarisha miundombinu ya barabara ili kuweza kusafirisha mazao toka mashambani kwenda kwenye masoko mbalimbali, suala ambalo pia litawavutia wawekezaji wengi zaidi.

Makonda ahakikisha Taifa Stars kupata ushindi, Rais amruhusu kwenda Misri kutoa motisha
Bakwata Kagera yaweka wazi mpango kazi wake wa miaka mitano