Fatma Karume, wakili anaeongoza jopo la mawakili takribani ishirini wanaomtetea Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) amesema kuwa suala la mteja wake kurejeshwa rumande baada ya kusomewa mashtaka linahitaji subira.

Karume aliyasema hayo jana, muda mfupi baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuamuru Lissu arudishwe rumande hadi Julai 27 ambapo uamuzi wa kumpa dhamana au la utatolewa na mahakama hiyo.

“Mimi nilishamuona Tundu amekaa ndani tangu Alhamisi, Ijumaa, Jumamosi na Jumapili… Kwakweli nimetoka I’m disappointed kwamba ningependa kumtoa leo. Lakini na hakimu pia ana haki kukaa kufikiri, kutafakari na kuandika maamuzi yake. Kwahiyo tutangojea hadi Alhamisi. Ni subira,” alisema Karume.

Mawakili wa upande wa Jamhuri waliiomba Mahakama kutompa dhamana mbunge huyo wa Singida Mashariki kwa madai kuwa upelelezi ulikuwa unaendelea na kwamba ana mashtaka mengi ya uchochezi yanayomkabili.

Lissu alikamatwa Alhamisi ya wiki iliyopita katika Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere alipokuwa akijiandaa kuelekea jijini Kigali nchini Rwanda kuhudhuria mkutano wa wanasheria wa Afrika Mashariki. Jeshi la polisi lilimfungulia mashtaka ya kutoa lugha ya uchochezi.

Video: Haijawahi kutokea, Werema afunguka kauli ya Tumbili
Magazeti ya Tanzania leo Julai 25, 2017