Siku mbili kabla ya mechi ya watani wa jadi kupigwa kwenye Dimba la Taifa, Dar es Salaam, Yanga imepiga hodi Simba na kuomba kuketi mezani kumaliza ‘bifu’ kati yao kuhusu mchezaji Hassan Kessy.

Yanga imefikia uamuzi huo wakati tayari muda uliowekwa na Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji kumaliza suala hilo ukiwa umekwisha.

Rais wa Simba, Evans Aveva, alisema wamepokea wito kutoka Yanga kuhusiana na sakata la mchezaji huyo wa zamani wa Simba.

Hata hivyo, Aveva alisema Simba bado inaendelea na msimamo wake wa kutaka makubaliano kufanyika kisheria na siyo kinyume chake.

“Kwa maelekezo ya kamati leo (jana) ndiyo ulikuwa mwisho wa sisi kumalizana, lakini Yanga imeomba tukutane kesho (leo) saa tano asubuhi ili kulimaliza sakata hili,” alisema Aveva.

Aliongeza: “Uamuzi wa Yanga kuomba kukutana na sisi, maana yake wameelewa malalamiko yetu na wako tayari kumalizana.”

Yanga imemua kupiga hodi Simba ili ipate baraka za kumtumia mchezaji huyo kwenye mechi ya Jumamosi wiki hii.

Simba iliwasilisha malalamiko mbele ya kamati iliyoko chini ya Mwanasheria Richard Sinamtwa wakidai kuwa klabu hiyo ya Jangwani ilimsajili Kessy aliyekuwa bado ana mkataba kucheza Msimbazi.

Kupitia madai hayo, Simba inataka kulipwa Dola za Marekani 600,000 (sawa na Sh. bilioni 1.2).
Kutokana na utata huo wa usajili, Yanga ilishindwa kumtumia Kessy katika mechi za hatua ya makundi ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambayo timu hiyo ilifuzu mwaka huu.

Kama muafaka wa kisheria wanaoutaka Simba utafikiwa, basi hapana shaka Kessy anaweza kuvaa jezi Jumamosi dhidi ya timu yake ya zamani.

 

Lipumba, Maalim Seif Uso kwa Uso Ofisini
Picha: Serengeti Boys Walipowasili Mjini Brazzaville