Suala la kuhamishia wakimbizi nchi ya tatu, kama njia mojawapo ya kutekeleza mkataba wa kimataifa wa wakimbizi linaendelea kuzaa matunda, ambapo shirika la uhamiaji la Umoja wa Mataifa linasema tangu mwezi Agosti 2021 limesaidia wakimbizi 20,000 kutoka Afghanistan kuhamia nchini Canada.

Taarifa ya IOM, iliyotolewa leo mjini Geneva, Uswisi inasema idadi hiyo imefikia baada ya Wakimbizi hao kuwasili mjini Toronto, Canada, kwa ndege kutoka Falme za kiarabu ikiwa na watu 337, miongoni mwao wakiwa ni watoto 121 walioambatana na maafisa wa IOM.

Kufuatia hatua hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa IOM, António Vitorino amesema, “jukumu la kuhamishia wakimbizi nchi ya tatu kwa njia salama na yenye utu, na suala hili limekuwa la IOM kwa zaidi ya miaka 70 sasa.”

Amesema, wanaendelea kushirikiana na serikali ya Canada na nchi nyingine kuhakikisha makumi ya maelfu ya waafghanistan walio hatarini wanapatiwa fursa ya kuanza upya maisha yao katika mazingira salama na yenye usaidizi.

IOM inasema ubia wake wa muda mrefu na serikali ya Canada imewezesha siku za awali kuhamishia nchini humo raia wa Syria na Ira, na kwamba “shirika hilo litaendelea kushirikiana na wadau wengine duniani kusaidia azma ya Canada ya kukubali angalau wakimbizi 40,000 kutoka Afghanistan.”

Pamoja na kuratibu ndege za kusafirisha wakimbizi hao, IOM inasema inawasaidia wakimbizi hao mchakato wa maombi na kuwapatia tathmini za uchunguzi wa kiafya kabla ya safari, sambamba na kuwaandaa na mafunzo ya jinsi wanavyoweza kuishi nchini Canada.

Mbatia avuliwa uanachama NCCR-Mageuzi
Siogopi, nikivurugwa nawavuruga: Chalamila