Imeelezwa kuwa asilimia kubwa ya wakulima wanashindwa kupiga hatua kupitia kilimo wanachofanya kwa kukosa utaalamu wa kanuni bora za Kilimo wakiendelea kung’ang’ania mashamba makubwa yasiyo na tija hali inayopelekea kubaki katia kilimo cha Jembe la mkono na kuanza moja kila mwaka.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Kampuni ya Agriculture Media, Raphael Jackson wakati wa semina iliyowakutanisha wajasiliamali, wakulima na wafugaji wa Manispaa ya Mtwara Mikindani ambapo amesema kuwa wakulima wengi hususani wadogo wanaotumia kilimo cha Jembe la Mkono wanashindwa kupiga hatua kiuchumi baada ya kulazimisha kulima mashamba makubwa.

“Mimi kinacho nisikitisha kwanini sasa mnang’ang’ania kulima mashamba makubwa wakati kila mwaka mavuno ndo yale yale, kama kweli tukitaka kukifanya kilimo kitutoe katika hali tuliyo nayo ni lazima kila mkulima achukulie shamba lake kama ofisi na sio kuendelea na mazoea kama tunavyofanya leo,”amesema Jackson

Nao baadhi ya wakulima waliohudhuria katika semina hiyo akiwemo Leah Amiri pamoja na Matha Njovu wamesema kuwa kinacho pelekea wengi wao kubaki katika hali waliyo nayo ni kukosa elimu juu ya namna ya kufanya kilimo cha kisasa pamoja na gharama za kununua Pembejeo zinazo endana na Kilimo hicho, ikiwemo madawa na Mbolea.

Kwa upande wao Wadau wa kilimo wakiwemo Taasisi za Kifedha wanasema hatua hiyo ya kuwajengea uwezo wakulima itasaidia kuwaongezea sifa za kupata dhamana ya mikopo kwani elimu hiyo imeenda sambamba na kuwahamasisha kujiunga katika vikundi ili kuwa na uwezo wa kukopesheka na hatimaye kuzalisha kwa tija malighafi zitakazo tumika viwandani.

Hatua hiyo ya kuwajengea uwezo wakulima wadogo imetajwa kuwa huenda ikasaidia kuwaondoa kutoka katika hali ya kilimo cha mazoea na kuelekea kulima kisasa kwa kufuata kanuni bora za Kilomo.

Dkt. Yonaz akabidhi Kompyuta mkoani Simiyu
Wananchi wajenga vyumba vitano vya madarasa wilayani Mtwara