Wakuu wa nchi za Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na mwenyeji wao, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli wanakutakana leo jijini Arusha kwa ajili ya Mkutano wao wa 20.

Marais wengine waliohudhuria ni pamoja na Yoweri Museveni (Uganda), Paul Kagame (Rwanda) na Uhuru Kenyatta (Kenya). Rais Pierre Nkurunzinza (Burundi) amewakilishwa na Makamu wake wa kwanza; na Rais Salva Kiir (Sudan Kusini) ambaye ni mualikwa pia akiwakilishwa na Waziri wa Biashara, Paul Mayon.

Mkutano huo ulikuwa ufanyike Novemba 30 mwaka jana, ulihamishiwa Disemba 27 lakini ulishindwa kufanyika pia kutokana na sababu kadha wa kadha zilizotolewa na baadhi ya nchi wanachama. Hatimaye, leo viongozi hao wamefanikisha kukutana kujadili ajenda husika.

Viongozi hao wanatarajia kujadili mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na mchakato ulianza muda mrefu la umoja wa forodha unaolenga kutafuta namna bora ya kuondoa ushuru kwenye mipaka ya nchi wanachama (non-tariff barriers). Wakuu hao wa nchi wanatarajia kujadili pia mchakato wa maombi ya Somalia kujiunga na umoja huo.

Ratiba rasmi ya mkutano huo iliyotolewa kwa vyombo vya habari imeonesha pia kuwa suala la shirikisho la kisiasa la Jumuiya hiyo litakuwa miongoni mwa ajenda.

Ajenda nyingine muhimu ni kuidhinisha hatua ya Kenya kuwania nafasi ya kuwa mjumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambacho ni chombo cha juu zaidi cha maamuzi kwenye Umoja huo.

Mkutano huo unatarajiwa kuanza leo majira ya adhuhuri.

NB: Picha ya habari ni kutoka maktaba; Mkutano wa 19 wa Wakuu wa Nchi za Afrika Mashariki uliofanyika jijini Kampala nchini Uganda.

Video: Makonda aanika ya wasanii, 'hakuna asiyejua mmefulia'
Video: Ukifika muda wako utumie, mtajuta - Manara